Prof. Ndalichako apeleka shangwe la Eid kwa watoto wenye ulemavu

Mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini Profesa Joyce Ndalichako leo amesherehekea sikukuu ya Eid el Fitri 2024 kwa kutoa zawadi mbalimbali ikiwemo vyakula kwa watoto wenye ulemavu wanaoishi na kusoma katika kituo cha Shule ya Msingi  Kabanga mazoezi wilayani Kasulu.

Akikabidhi misaada na vyakula kwa ajili ya sikukuu ya Eid pamoja na sabuni za zana nyingine kwa ajili ya usafi, Profesa Ndalichako ameeleza kuwa amefanya hivyo ili kuonesha upendo kwa watu wenye mahitaji maalumu hususani watoto ambao wamelazimika kutokuwepo nyumbani kwao wakati wa sikukuu 

"Leo ni sikukuu na mimi kama Mbunge wenu nimeona ni vema niungane nanyi katika sikukuu hii kwa kuwaletea zawadi kidogo ili nanyi mfurahie kama watoto wengine" ameeleza Profesa Ndalichako wakati akikabidhi misaada hiyo kwa watoto wenyewe.

Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na jumuiya ya wanafunzi, walimu, watumishi wengine na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi katika shule ya msingi mazoezi kabanga kabla ya kutoa zawadi ya sikukuu ya Eid el Fitri mpema leo

Amekiri kuwa watoto hao wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na hali ya maumbile yao, kuishi mbali na jamii yao hususani wazazi, ndugu, jamaa na marafiki na anawatia moto kuwa ulemavu si mapungufu ya kuwazuia kutimiza malengo yao na kwamba mafunzo wanaopata katika kituo hicho yatawawezesha kuwa watu mhimu katika jamii

Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Mazoezi Kabanga baada ya kukabidhi misaada mbalimbali kwa ajili ya sikukuu ya Eid el Fitri Mjini Kasulu

"Kuwa na ulemavu siyo mapungufu ya kushindwa kufikia yale mnayoyatamani, naomba msome kwa bidii na muwe na nidhamu, mwisho wa siku mtaweza kuzifikia ndoto zenu, naamini walimu wenu wanafanya kazi nzuri na wanawapenda, Mkurugenzi wa Halmashauri ni mgeni lakini anafuatilia ili kujua mahitaji yenu na naamini atawaweka katika mipango yake" Amesisitiza Profesa Ndalichako

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Miji wa Kasulu Bw. Vumilia Simbeye amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kasulu Prof. Joyce Ndalichako kwa uamuzi wake wa kutoa zawadi hususani vyakula na zana za usafi kwa watoto hao na kutoa wito kwa viongozi wengine kutambua mahitaji ya wenye ulemavu na kusaidia serikali katika kuwahudumia

Ndugu Vumilia Simbeye Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kasulu akihutubia watoto na walezi wao katika shule ya msingi Kabanga mazoezi kabla ya kumkaribisha mbunge wa jimbo la kasulu mjini Prof. ndalichako kukabishi zawadi kwa watoto wenye ulemavu.

Bw. Simbeye amebainisha kuwa serikali kupitia Halmahsuri ya Mji itaendelea kuhakikisha watoto hao zaidi ya 150 wanapata huduma stahiki ikiwemo ulinzi na elimu.

"Ninatambua kuwa watoto hawa wanahitaji usaidizi wetu na tutahakikisha wanapata huduma zote, pamoja na ugenzi wangu nimefurahi kufika katika shule na kituo hiki na kujionea maisha ya watoto wetu, namshukuru Mbunge kwa kunishirikisha katika sikukuu hii kufuarahia nanyi, mimi nami ninajipanga na nitakuja siku nyingine" Amesisitiza Vumilia Simbeye Mkurugenzi mpya wa halmashauri ya mji wa Kasulu 

Jamii ya wanafunzi, watoto wenye ulemavu na uongozi wa shule na kituo cha wenye ulemavu Kabanga wametoa shukurani kwa mbunge wao huku wakimwahidi kuendelea kumuunga mkono katika hatarkati zake za uwakilishi.

Profesa Joyce Ndalichako (MB) akitoa maelekezo kwa afisa elimu maalumu Mwl Kitogwe kuhakikisha anawasilisha taarifa za hali ya ulemavu wa watoto kwa mamlaka za serikali ili hatua zaidi za usaidizi kwa wenye ulemavu wa viungo zichukuliwe, Katikati ni mkurugenzi mpya wa halmashauri ya mji Kasulu Bw. Vulimia Simbeye akisikiliza kwa umakini maelekezo ya mbunge kwa afisa elimu maalumu.

Prof. Joyce Ndalichako (MB) katika picha na baadhi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi wanaoishi katika kituo cha shule ya msingi Kabanga mazoezi kama sehemu ya hifadhi kwa ajili ya ulinzi na pia shule kwa ajili ya kuwapatia elimu ya msingi, mbele yao ni baadhi ya misaada aliyowakabidhi katika kusherehekea sikukuu ya Eid el Fitri 2024

Hatua hii ya utoaji wa msaada wa chakula cha sikukuu kwa watoto wenye ulemavu imetanguliwa na Mbunge huyo kutoa zawadi mbalimbali kwa waislamu katika misikiti takribani 44 ndani ya Jimbo la kasulu mjini pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali hususani wanawake, wazee na wagonjwa na kufururisha viongozi wa kijamii na chama wakati wa mfungo mtukufu wa Ramadhani.

Profesa Joyce Ndalichako (MB) akiimba na kucheza na watoto wenye Ulemavu pamoja na viongozi wengine wa jamii kata ya Msambara, Kushoto mwenye suti nyeuzi ni mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa kasulu Bw. Vumilia Simbeye ambaye pia aliungana na mbunge na watoto hao kuimba na kucheza

Prof. Joyce Ndalichako (mwenye nguo ya njano katikati) akiwa na viongozi mbalimbali wa mitaa, kata na halmahsuri ya mji baada ya kukabidhi misaada kwa watoto wenye mahitaji maalumu. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa kasyly Bw. Vumilia Simbeye

Sikukuu ya Eid el Fitri husherehekewa baada ya takribani siku thelathini za mfungo mtukufu wa ramadhani kwa waumini wa madhehebu ya kiislamu kote duniani, ambapo waumini wanafunga vyakula kwa ajili ya Sala na maombi ya Neema kwa Mwenyezi Mungu.




Post a Comment

0 Comments