Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) limetumia kiasi cha Sh.270 milioni kwa kituo cha afya cha Ilagala, wilayani Uvinza mkoani Kigoma,
kwa ajili ya ukarabati wa jengo la kliniki ya tiba na matunzo kwa wenye virusi
vya UKIMWI, pamoja na vifaa tiba na samani.
Hafla ya makabidhiano ya jengo hilo imefanyika jana katika Kituo cha
Afya cha Ilagala, ambapo Mkurugenzi wa Miradi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia
Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC )Tanzania, Dkt. George Mgomella akiambatana na
Mkurugenzi Mtendaji wa THPS, Dkt. Redempta Mbatia wamekabidhi jengo hilo, samani na vifaa vya
uchunguzi na kinga ya saratani ya mlango wa kizazi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,
Mhe. Thobias Andengenye aliyewakilishwa na mganga mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba.
Ukarabati huo uliogharimu jumla ya Shilingi milioni 211, ulihusisha urekebishaji wa vyumba mbalimbali vya matibabu ndani ya jengo hilo, vikiwemo vyumba vya ushauri nasaha, chumba cha usajili, maabara, chumba cha kutolea dawa, sehemu ya kusubiria huduma na chumba cha kutunza kumbukumbu za matibabu.
Dr. Mgomella alibainisha kuwa uboreshaji wa jengo hilo pamoja na vifaa tiba ambao umefanyika kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiriana na UKIMWI (PEPFAR) na U.S. CDC kupitia mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika la THPS, utasaidia kuwepo kwa mazingira mazuri zaidi ya utoaji wa huduma bora za afya hususani tiba na matunzo kwa wapokea huduma wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Dkt. George Mgomella Mkurugenzi wa Miradi wa U.S. CDC Tanzania akihutubia wakati wa hafla ya
kukabidhi jengo la CTC, katika
kituo cha Afya Ilagala, wilayani Uvinza
Dkt.
Mgomella alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika mapambano dhidi ya VVU na
UKIMWI huku akipongeza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, viongozi wa mkoa wa Kigoma, mamlaka za
serikali za mitaa na Shirika la THPS kwa dhamira yao thabiti ya kutoa huduma
bora za afya kwa wananchi.
"Ukarabati uliofanyika, sio
tu utaboresha
huduma zinazotolewa lakini pia mazingira ya kutolea huduma yatavutia jamii
kufika na kupata huduma katika kituo hiki", alisema Dr. Mgomela.
Jengo la huduma na
matunzo kwa wenye maambukizi ya VVU lililokarabatiwa na THPS katika kituo cha
afya Ilagala mkoani Kigoma
Sambamba na
jengo lililofanyiwa ukarabati, CDC na THPS pia walikabidhi mashine tatu za ‘Thermocoagulation’ na
zingine tatu za ‘Cryotherapy’ ili
kusaidia utambuzi na matibabu na kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa
wasichana mkoani Kigoma.
Mashine
hizo, zenye thamani ya jumla ya Sh. 58.7 milioni
zitasaidia katika kutoa huduma na kuokoa maisha kwa wanawake waliopo katika
eneo hilo na kusaidia utekelezaji wa mpango wa taifa wa kupambana na saratani
ya mlango wa shingo la kizazi.
"Tunaamini
kwamba kwa kuwekeza katika teknolojia hizi za kiwango cha juu, tunaweza
kuchangia katika kuokoa maisha wa walengwa", alisema Dkt. Mgomella.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa THPS Dkt Redempta Mbatia amepongeza uwepo
wa sera nzuri za afya ndani ya Serikali
ya Tanzania akieleza kuwa sera hizo ndizo zimechochea serikali ya Marekani
kutoa ufadhili mkubwa katika miradi ya afya nchini Tanzania.
“Tukumbuke kuwa kama sio sera Madhubuti za
Serikali yetu, hata ufadhili huu tusingeupata”, alisema Dkt. Mbatia.
Dkt. Mbatia alibainisha
kuwa kupitia mradi
wa Afya Hatua THPS inatoa huduma za afya za kinga
na matibabu kwa wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi katika vituo 67 vya afya
mkoani Kigoma.
Alieleza
kuwa pamoja na huduma za kinga, na tiba THPS imewezesha mkoa kuajili watumishi
wapatao 262 ambapo kati yao 22 wameajiriwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Kigoma, na
kwamba tangu mwaka 2011 THPS na serikali ya mkoa wa Kigoma wamewafikia watu
wenye virusi vya Ukimwi 51,757
ambapo 22,086
kati yao wapo kwenye
matibabu ya VVU na 99% wamefubaza virusi vyao.
Hata
hivyo Dkt Mbatia ametahadharisha kuwa pamoja na kwamba jitihada hizi zimesaidia kupunguza maambukizi
ya VVU katika mkoa wa Kigoma hadi 1.7% ukilinganisha na mwaka 2017 ambapo maambukizi yalikuwa 2.9%, bado kuna idadi kubwa ya vijana
ambao
hawajitokezi kupima afya zao.
Akizungumza katika hafla hiyo mkuu wa mkoa wa Kigoma Mhe. Andengenye
kupitia katika hotuba yake iliyosomwa na mganga mkuu wa mkoa wa Kigoma Dkt.
Jesca Lebba alitoa shukrani zake za dhati kwa msaada unaotolewa na serikali ya
Marekani kupitia CDC na THPS katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI mkoani
Kigoma.
Mhe. Andengenye aliahidi kudumisha ushirikiano na CDC na THPS ili
kuendelea kuokoa maisha na kudhibiti VVU na UKIMWI katika mkoa huo. Mhe.
Andengenye alipongeza ushirikiano na jitihada kubwa za wadau katika vita dhidi
ya VVU.
“Kituo hiki ni muhimu sana katika kutoa huduma za afya katika eneo hili,
na naamini kuwa maboresho yaliyofanyika yataongeza motisha kwa wahudumu wa afya
katika kuhudumia jamii yetu", alisema.
Mradi
wa CDC/PEPFAR Afya Hatua ni uthibitisho wa juhudi za ushirikiano za wadau wa
ndani na kimataifa wanaohusika katika utekelezazi wa afua mbalimbali
zinazolenga kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya.
“Naomba
mhakikishe kituo hiki na vifaa vilivokabidhiwa vinatumika ipasavyo na kutunzwa
vizuri, ili kuhakikisha kuwa wananchi wa eneo hili wanaendelea kupata huduma bora za afya, na
pia kuweza kuzuia ipasavyo saratani ya mlango wa kizazi na hivo kuokoa maisha,”
alisema.
Pamoja
na shukurani hizo, Mhe.
Andengenye ameomba THPS kuendelea kusaidia juhudi za serikali za kuporesha
huduma za afya ikiwemo kuanzisha huduma za tiba na matunzo kwa wenye VVU katika zahanati za
Businde, Msufini na Rungwe mpya sambamba na kutoa mafunzo kwa wahudumu wapya wa afya kuhusiana na kuzuia
maambukizi ya VVU kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo walikiri kuwa eneo lao limekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za CTC kutokana na jiografia yake ambapo walilazimika kuifuata huduma hiyo zaidi ya kilimota 100 kwenda Hospitali ya wilaya iliyoko makao makuu ya wilaya ya uvinza
Hassan Nona na Zuwena Abubakar ambao ni wakazi wa Ilagala wameiambia Buha News kuwa kutokuwepo na kituo cha kisasa cha CTC kulipelekea waliobainika kuwa na maambukizi kukosa hudama bobevu na kupelekea wengi wao kuacha kuhudhuria kituoni hapo
"Kutokana na huduma kupatikana mbali na eneo letu wapo wanaoishi na VVU walioamua kujificha au kusitisha kupata huduma zinazotakiwa lakini kwa ukarabati huu uliofanywa na THPS pamoja na vifaa ambavyo vimewekwa tuna imani kuwa watu wengi zaidi watajitokeza kupima na watakaokutwa na maambukizi watapata huduma" alisisitiza Zuweza
Kwa upande wake Hassan Nona alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa vijana kujitokeza kupima afya zao na kuepuka tabia ya kuwaweka wanawake kama kinga kwao kukwepa kupima na kutekemea majibu ya vipimo vya wake zao wanapokuwa na ujauzito
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mganga Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Mganga Mkuu wa Wilaya, Watumishi wa Kituo cha Afya Ilagala, Maafisa wa THPS na wananchi wa Uvinza walihudhuria na kushuhudia tukio hilo muhimu.
Kuhusu THPS
Tanzania Health Promotion Support (THPS) ni asasi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa mwaka 2011, chini ya Sheria ya asasi zisizo za kiserikali nambari 24 ya 2002.
THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya Jinsia, Vijana, Wazee na Makundi Maalum; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada ya UKIMWI kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU/UKIMWI; Kifua kikuu; kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto; huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa afya, na UVIKO-19.
Kliniki ya Tiba na Matunzo ya Kituo cha Afya cha Ilagala wilayani Uvinza, Kigoma imefanyiwa marekebisho makubwa kupitia mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika laTanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR), kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).
Kuhusu mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua
(Oktoba, 2021- Septemba, 2026)
Mradi huu
unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya afya (Kigoma, Pwani, Shinyanga
na Tanga) na katika jamii (Kigoma, Pwani na Tanga).
Huduma hizi ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga na programu ya DREAMS kwa wasichana balehe na wanawake wadogo katika mkoa wa Shinyanga.
Mwandishi: Prosper Kwigize
Mhariri: Adela Madyane
0 Comments