DC Kasulu Kanali Mwakisu apongezwa kwa kudhibiti kamchape

Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu apongezwa kwa kufanikisha udhibiti wa kikundi cha Kamchape ambacho kinahusishwa na uporaji na uchonganishi katika jamii mkoani Kigoma.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mh. Eliya Kagoma wakati wa kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika leo katika makao makuu mapya ya halmashauri hiyo eneo la Nyamyusi.

Mh. Kagoma amebainisha kuwa kikundi cha Kamchape kimekuwa tishio la Amani kwa jamii wilayani humo na kimekuwa kikisababisha uvunjifu wa Amani sambamba na uporaji wa mali za wananchi

“Licha ya kwamba Kamchape wamekuwa wakipora mali za watu, wamesababisha chuki miongoni mwa jamii kutokana na kupandikiza Imani za kishirikina na kusababisha jamii kutoaminiana” Anasema Mhe. Eliya Kagoma

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mhe. Eliya Kagoma ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kitanga akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani mapema leo. Picha na. Prosper Kwigize - Buha News

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kasulu kanali Isack Mwakisu ametumia kikao hicho kuendelea kutoa wito kwa jamii wilayani humo kukataa ushawishi wa kamchape na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola endapo watawabaini watu wanaijihusisha na kikundi hicho

Amewataka madiwani kutumia nafasi zao kutoa elimu kwa jamii kuhusu kuepuka vitendo vya kishirikina vinavyochochea uvunjifu wa Amani na kuzorotesha maendeleo


Vikundi vya watu wanaofahamika kwa jina la rambaramba au kamchape vimekuwa tishio mkoani Kigoma kutokana na mwenendo wao wa kuaminisha jami kuwa watu Fulani wanamiliki uchawi na kwamba wanao uwezo wa kuondoa uchawi huo lakini wanapotekeleza kazi hiyo ufanya uhalifu ikiwemo wizi na kuchochea chuki miongoni mwa jamii

Watu kadhaa wameripotiwa kupoteza maisha katika vurugu za kikundi cha kamchape huku makumi wengine wakikamatwa na jeshi la polisi kwa kusababisha uvunjifu wa Amani, uharibifu wa mali, uporaji na wizi.

Wakati huo huo mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu ametumia kikao cha madiwani kuwataka Viongozi wa kijamii, vyama vya siasa pamoja na madiwani kuepuka vitisho dhidi ya wananchi wanaoonesha nia ya kugombea uongozi wa serkali za mitaa utakaofanyika mwezi Oktoba 2024.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu wakishiriki Kikao cha Baraza kilichokuwa na jukumu la kupokea taarifa mbalimbali za maendeleo


Ameonya kuwepo kwa kuwepo kwa kampeni za mapema zinazoenda sambamba na upangaji wa safu kupitia vikundi vya wanasiasa, akihimiza kuzingatiwa kwa miongozo ya kisheria huku akihimiza kuwa muda utakapofika wenye sifa za kugombea wapewe nafasi na haki ya kushiriki uchaguzi huo.

Mwandishi: Prosper Kwigize

Mhariri: Adela Madyane

 


Post a Comment

0 Comments