Wananchi wapaza sauti juu ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto


Idadi ya watoto waliotelekezwa na kufanya kazi za mtaani mkoani Kigoma imepungua kutoka 987 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia watoto 845 kwa mwaka 2022/2023.

Takwimu hizo zimetokewa Leo tarehe 15 Mei 2024 na afisa ustawi wa jamii mkoa wa Kigoma Petro Mbwanji wakati wa kongamano la kilele cha maadhimisho ya siku ya familia ambayo kimkoa yamefanyika katika halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mbwanji amesema takwimu hizo zimepungua kutokana na uelewa wa wananchi juu ya matukio ya kikatili yanayofanywa katika ngazi ya familia na kuyatolea taarifa ili yafanyiwe kazi na mamlaka husika.

Afisa ustawi ametaja sababu za kutelekeza watoto kuwa ni pamoja migogoro katika ndoa inayowafanya wazazi kuachana na watoto kukimbilia mtaani na kuwa ombaomba kwasababu ya kukosa uangalizi.

“Tunaendelea kuielimisha jamii juu ya kutimiza wajibu wao katika malezi, wazazi walee watoto wao sawasawa na miongozo ya serikali, na watoto watekeleze wajibu wao ili tupate jamii iliyo nzuri”. Amesema Mbwanji.

Kwa upande wa viongozi wa dini Michael Kulwa mwenyekiti wa makanisa ya Kipentekoste mkoani humo ameitaka jamii kusimamia maadili ya ki Mungu na kupata watoto ndani ya ndoa ambao watatelewa katika misingi ya mizuri ya imani na kwamba sio rahisi kwa wazazi kuachana na kukimbia majukumu yao.

Naye Anna Dasrin mkazi wa Mwasenga amesema ili kuondokana na changamoto ya watoto wa mtaani baadhi ya wazazi wakiume lazima wawajibike kwa watoto wao kwani wengi wao wamekuwa wakishinda kwenye vijiwe vya kahawa na vya siasa na kuwaachia majukumu wake zao.

Zabibu Amrani mke wa tatu kwa mume wake (jina limehifadhiwa) amesema ndoa za mitara zinachangia kwa kiasi kikubwa watoto kuzagaa mtaani kwani wanakuwa sehemu ya kutafuta pesa kwaajili ya familia zao hasa kwa mama zao ambao hawahudmiwi ipasavyo na waume zao.

Akizungumza Michael Mgema, mkuu wa dawati la jinsia na watoto, amesema jumla ya makosa ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto yaliyotolewa taarifa kwa kipindi cha Januari hadi Disemba 2023 ni 1547 na kutaka jamii iendelee kushirikiana kwa pamoja ili kupinga vitendo hivyo nankuvitolea taarifa ili kuepusha muendelezo wa matukio hayo ya kikatili. 

Mwandishi: Adela Madyane

Mhariri: Prosper Kwigize 

Post a Comment

0 Comments