Kasulu DC wahamia katika majengo mapya - Madiwani wapongezwa

Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kasulu limeanza kufanya shughuli zake rasmi katika majengo mapya ya makao makuu ya halmashauri hiyo yaliyongengwa katika eneo la Nyamyusi na Nyakitonto wilayani humo.

Akihutubia baraza hilo mapema jana, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mh. Eliya Kagoma alipongeza na kuishukuru serikali kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa jengo la halmashauri hiyo na kusisitiza kuwa sasa shughuli zote za serikali ngazi ya halmashauri hiyo zitafanyika ketika eneo hilo.

Mh. Kagoma alisisitiza kuwa tangu halmashauri zilipogawanywa na kuunda halmashauri mbili za Kasulu mji na Kasulu DC, sehemu yake imekuwa ikifanyia shughuli zake katika majengo ya kuazima jambo ambalo lilipunguza ufanisi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Ndg. Eliya Kagoma akitangaza msimamo wake wa kuhamia katika majengo rasmi ya serikali.

"Mimi kuanzia leo nimehamia hapa, kule Nyakitonto sitarudi tena, na kwa msimamo huu nawaagiza wakuu wa idara na watumishi wote kuhamishia ofisi zenu hapa ili kutekeleza wajibu wenu kwa ufanisi zaidi" alisisitiza Mh. Kagoma

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu alitumia Baraza hilo kuwapongeza madiwani kwa kufanikisha ujenzi wa jengo la kisasa la halmashauri na kutoa wito kwa kulitunza na kulitumia kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu (kushoto) akizikiliza kwa umakini msimamo wa mwenyekiti wa halmashauri kuhusu kuanza kutumika kwa jengo jipya la halmashauri hiyo.

Hata hivyo Kanali Mwakisu aliwataka madiwani kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia miradi ya maendeleo katika kata zao na kuadha dhana kuwa ni miradi ya serikali kuu

Anasema kuwa katika ufuatiliaji wake amebaini kuwa madiwani hawakagui wala kusimamia miradi jambo linalochangia kuwepo kwa ubadhilifu au uzembe unaozorotesha utekelezaji wa miradi husika

"Ninashangaa, ninyi ndio mnaopanga miradi hiyo na kutenga bajeti, lakini utekelezaji unapoanza hamfuatilii, unaenda kukagua unakuta kitabu cha wageni kuna jina la DC au mkuu wa mkoa lakini diwani unayeishi katika kata hiyohiyo hujawahi kutembelea mradi, hii si sawa. Alisisitiza Kanali Mwakisu

Jengo jipya la makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Kasulu ambapo kwa mara ya kwanza shughuli za baraza zimeanza kulitumia May 09, 2024

Madiwani kwa pamoja walikubaliana na hoja wa mkuu wa wilaya na kupitia kwa mwenyekiti wao waliahidi kuwa watafuatilia na kusimamia miradi yote ya umma katika maeneo yao.

Wilaya ya Kasulu ni miongoni mwa maeneo yenye miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa shule, zahanati, miundombinu ya barabara na maji. 


Post a Comment

0 Comments