Kijiji cha Katoto wilayani Kasulu kuhamishwa kupisha hifadhi ya mazingira


Serikali ya Tanzania inatarajia kukihamisha Kijiji cha Katoto kilichopo ndani ya bonde la mto Malagarasi wilayani Kasulu ili kupisha uhifadhi wa bonde la ardhi oevu na ramsa ya Mto Malagarasi ambao uko hatarini kutoweka kutokana na uvamizi wa wakulima na wafugaji

Azimio hilo la Baraza la Mawaziri limewasilishwa na mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu wakati akihutubia Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma

Akinukuu maagizo ya Baraza la Mawaziri Kanali Mwakisu amebainisha kuwa wakazi wa Katoto ambao ni wafugaji watapewa ardhi mpya jirani na kijiji cha Kagerankanda katika eneo la sehemu ya kitalu cha uwindaji ili kuanzisha makazi mapya.

“Baada ya tafakari ya muda mrefu inayoenda sambamba na kubaini athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoukabiri mto malagarasi ambao unachangia asilimia 70 ya maji yanayoingia katika ziwa Tanganyika, serikali sasa itakihamisha kijiji cha Katoto ili kupisha uhifadhi wa ramsa ya bonde la Malagarasi ambayo inatambuliwa kimataifa” Alisisitiza Kanali Mwakisu

Mkuu huyo wa wilaya amewataka madiwani na viongozi wa serikali katika halmashauri hiyo kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa azimio la kukihamisha kijiji hicho huku akibainisha kuwa taratizo zitakapokamilika wananchi wa kijiji hicho wataarifiwa na kuandaliwa kwa ajili ya kuhama.


Wakati huo huo Mkuu wa wilaya ya Kasulu amewatangazia wananchi wa wilaya hiyo kuwa serikali inatarajia kuhakiki na kupima mipaka ya ardhi na hifadhi ya misitu katika wilaya hiyo ili kumaliza migogoro ya ardhi baina ya wakulima, wafugaji na serikali

Baadhi ya madiwani wakifuatilia kwa umakini hotoba ya Mkuu wa wilaya kanali Mwakisu kuhusu migogoro ya aridhi na kuondolewa kwa kijiji cha Katoto katika eneo la ardhi Oevu ya mto Malagarasi. Picha na Prosper Kwigize- BUha News

Akihudubia katika baraza la madiwani Kanali Mwakisu amebainisha kuwa kumekuwepo na migogoro ya muda mrefu inayotokana na wananchi kuvamia ardhi katika hifadhi za misitu katika eneo la Kagerankanda na Mvinza pamoja na eneo la Makere kusini na Kaskazini hali inayosababisha uharibifu mkuwa wa mazingira.

“Tunatambua kuwa lipo tatizo kubwa la migogoro ya aridhi inayotokana na kutofahamika kwa mipaka rasmi katika maeneo ya hifadhi na vijiji, hivyo serikali imeandaa utaratibu wa kuhakiki mipaka na pia kupima upya baadhi ya maeneo yenye migogoro” Amesema kanali Mwakisu

Amebainisha kuwa licha ya wakulima kupewa ardhi yenye ukubwa wa hekta 10000 na aliyekuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania hayati Dr. John Magufuli wananchi wameendelea kuingia na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yasiyoruhusiwa na kusababisha migogoro

Kuhusu wananchi waliolima ndani ya hifadhi za misitu kuomba kibali cha kuvuna mazao yao, kanali Mwakisu amebainisha kuwa hana mamlaka ya kutoa kibali cha kufanya hivyo, huku akiwashangaa wananchii ambayo waliingia kinyemela hifadhini kulima bila vibali na sasa wanaomba kibali kwenda kuvuna

Kufuatia kuwepo kwa zuio la kisheria kwa mwananchi yeyote kutoruhusiwa kuingia katika hifadhi za taifa, kanali Mwakisu amewataka madiwani kutoa elimu kwa wapiga kura wao na kuepuka kuwachonganisha na serikali.

Madiwani katika halmashauri hiyo wamemhakikishia mkuu huyo wa wilaya kutoa ushirikiano wa dhati kwa kuwaelimisha wananchi kutovunja sharia za ardhi na hifadhi za misitu.

Mwandishi: Prosper Kwigize

Mhariri: Adela Madyane


Post a Comment

0 Comments