TUCTA Kigoma yaiomba serikali kuboresha maslahi ya wastaafu


Wakati watumishi wa umma waliostaafu zamani wakilia na maisha magumu na maslahi duni kutoka kwa serikali, Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoa wa Kigoma limeiomba serikali kuwatazama na kuwajali wastaafu wa zamani ambao bado wanalipwa shilingi laki moja kwa mwezi na kuwapa posho inayolingana na hali ya maisha.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi, (Mei mosi) kupitia hotuba iliyoandaliwa na chama hicho, katibu wa TUCTA, Jumanne Magulu ametaja kuwa wastaafu hao wanaishi maisha magumu kutokana na hali ngumu ya uchumi na kupanda bei kwa bidhaa.


“Tunaomba serikali iwatazame kwa upya wastaafu hao, iwakumbuke na kuwaongezea kiwango cha fedha ili waweze kujikimu na kukidhi mahitaji yao, laki moja ni pesa kidogo ambayo kwa maisha ya sasa haiwezi kuwasaidia kwa muda mrefu na kuwafanya waishi maisha magumu” amesema Magulu.


Katibu wa TUCTA mkoa wa Kigoma, ndg. Jumanne Magulu akisoma risala ya wafanyakazi
Picha na. Sara Mataro

Pamoja na hayo, TUCTA wameziomba pia taasisi za kifedha kupunguza kiwango cha riba ya mikopo ambapo wamesema kiwango hicho ni kikubwa na wapo ambao hawawezi kumudu kulipa.


Wafanyakazi hao wametumia Mei Mosi kuiomba mifuko ya hifadhi za jamii kufuatilia michango ya wanachama katika taasisi husika ili kuepusha changamoto ambazo huwa zinatokea kati ya mwajiri na mwajiriwa hasa katika kipindi cha kufuatilia mafao ambayo yalikuwa hayafikishwi katika mfuko.


Akizungumza Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewaasa wafanyakazi wote kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kubadili mienendo ya utendaji kazi, uwe wa juhudi na wenye maarifa ili kuinua uchumi wa nchi.


Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akiwahutubia wafanyakazi katika kilele cha siku ya wafanyakazi mkoa wa Kigoma katika uwanja wa Umoja Kasulu. 
Picha na. Sara Mataro

Amehimiza ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi wote na kuachana na tabia ya ubinafsi ambayo inafanya watu kukosa haki zao huku ikichochea rushwa na utovu wa nidhamu na hivyo kuharibu utendaji kazi kwa maendeleo.


Andengenye amesema, kufuatia suala la ongezeko la mishahara ambayo ndio kauli mbiu ya maadhimisho hayo kuwa serikali inafanyia kazi mapitio ya sheria ambazo  zinakandamiza maslahi ya wafanyakazi hivyo wawe wavumilivu mpaka pale serikali utakapokamilisha mapokeo hayo.


Amewaasa kuanzisha SACCOS ambayo itawaweseha kukopa kwa bei watakayojipangia kwani wao ndio wanao ndio wamiliki wakuu wa chanzo hicho cha fedha ili kuepukana na tiba kubwa kutoka kwenye taasisi za kifedha.


Baadhi ya wafanyakazi waliohudhuria kilele cha siku ya wafanyakazi mkoa wa Kigoma. 
Picha na. Sara Mataro

Hata hivyo, amewaonya waajiri wanaowanyanyasa na kuwakandakiza waajiriwa, amewataka wafanye kazi kwa kufuata sheria mpya na kutekeleza haki na wajibu wa kazi, na kwamba waajiriwa wasisite kutoa taarifa kwa waajiri wa namna hiyo ili waadhibiwe sawasawa na kanuni na sheria za nchi.


Lusajo Adamu kutoka shule ya msingi Kagina iliyopo halmashi ya wilaya ya Kigoma, ameiomba serikali iboreshe miundombinu ya shule sambamba na kurekebisha kikokotoo kiwe kwa asilimia 50 tofauti na ilivyo sasa.


Baadhi ya wafanyakazi wakicheza na kuimba kuashiria mchikamano miongoni mwao, ni katika uwanja wa CCM Umoja Kasulu. Picha na. Adela Madyane

Siku ya wafayakazi duniani huadhimishwa tarehe Moja mwezi mei kila mwaka ambapo wafanyakazi na waajiri wao hususani Serikali hukutana kujadili na kutaathimini ya uwajibikaji wa kila upande ikiwa ni pamoja na wafanyakazi kudai haki na maslahi kutoka kwa waajiri wao.


Mei Mosi Kitaifa mwaka huu nchini Tanzania imefanyika Mjini Arusha ambako mgeni rasmi alikuwa makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye ameahidi kuwa serikali itaongeza mishahara ya wafanyakazi kulingana na namna uchumi wa taifa unavyoboreka


Dkt. Mpango amebainisha hatua zinazotekelezwa na serikali kwa sasa ni kupandisha vyeo na madaraja watumishi wa umma ambapo zaidi ya bilioni 200 zimetengwa kwa ajili hiyo.


Mwandishi: Adela Madyane

Mhariri:    Prosper Kwigize


Post a Comment

0 Comments