Uvuvi ziwa Tanganyika wasimamishwa kwa kipindi cha miezi mitatu

Shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika leo zimesitishwa kwa nchi zote kwa lengo la kuongeza uzalishaji zaidi wa samaki sambamba na kudhibiti uvuvi haramu katika ziwa hilo linalotegemewa na chin nne za ukanda wa SADC na EAC

Hayo yametangazwa na mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli wakati akizungumza na waandishi wa habari mkjini kigoma kuhusu uamuzi wa serikali za nchi nne kusitisha shughuli za uvuvi katika ziwa hilo

Amefafanua kuwa uamuzi huo ni utekelezaji wa mpango mkakati serikali za Tanzania, Burundi, DRC na Zambia kudhibiti uvuvi usio endelevu

Mh. Kalli ameeleza kuwa shughuli za uvuvi wa dagaa umekuwa wa kiwango cha chini kutokana na kupungua kwa rasilimali hizo na kwamba uamuzi wa kusitisha shughuli hizo umelenga kuboresha mazao ya uvuvi

"Lengo la serikali zetu zinazozunguka ziwa Tanganyika ni kulipumzisha ziwa hilo ili samaki na dagaa wapate nafasi ya kuzaliana na hivyo tutakaporuhusu uvuvi kuendelea kuwepo na tija kwa kuvua samaki wenye ubora  tofauti na ilivyo kwa sasa" amesisitiza DC Salum Kalli 

Tangazo hilo licha ya kuzoeleka miongoni mwa wavuvi, mkoani Kigoma linaendelea kuzua sintofahamu kwa jamii ambayo sehemu kubwa kitoweo chao kikuu ni samaki

Wakizungumza na Buha News, baadhi ya wananchi wa mjini Kigoma wameeleza kuwa, lidha ya nia ya serikali kuwa njema lakini inawapa wakati mgumu kutokana na jamii kuzoea kula kitoweo cha samaki.

Bi. Veronica Kachacha anaeleza kuwa ipo hofu ya kuibuka au kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu kutokana na kundi kubwa la jamii hasa wanaume kutegemea shughuli za uvuvi pekee kwa ajili ya kuongeza kipato

"Tunaunga mkono uamuzi wa serikali maana tunaona nia yao ni nzuro lakini inabidi waongeze ulinzi maana tutaanza kukabwa na kuporwa mali zetu na wahalifu" Amesisitiza Bi. Kachacha 

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kusitisha shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika kupisha ongezeko la samaki, wakati kwa serikali za Burundi, DRC na Zambia wanatekeleza mkakati huo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2023.

Mwandishi: Prosper Kwigize
Mhariri: Adela Madyane

Post a Comment

0 Comments