Waathirika wa mafuriko mjini Bukoba wapata misaada ya kiutu

Wadau wa group la Whatsapp la  Bukoba mjini mpya kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Adv Stephen Byabato wametembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa waanga wa mafuriko yaliyotokea usiku wa kuamkia  Mei 9 mwaka huu katika kata saba za  Manispaa ya Bukoba.

Wadau hao wamefika katika kata hizo  ambazo zimeathiriwa na mafuriko hayo na kutoa vitu mbalimbali ikiwemo Mchele,Unga,Mafuta, Sabuni,Maharage na nguo kwa ajili ya kuwasaidia waanga hao kupata mahitaji hayo muhimu ambapo kila kata kaya 15 zimepatiwa msaada huo.

Baadhi ya wadau wa group hilo Jamila Emily,Erick Bashabi ,Sharifa Karwani ,Asimwe na Husna wamesema kuwa waliopata mafuriko wanahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo hivyo kwa umoja wao waliona ni vyema kuungana kwa pamoja  kuchangishana kama wana group ili kuwasaidia waanga hao .

Wameongeza kuwa group hilo limekuwa na utaratibu wa kushirikiana kwa pamoja  katika mambo mbalimbali yanayoigusa jamiii hivyo hata waanga wa mafuriko yaliyotokea manispaa ya Bukoba ni vyema wakasaidiwa .

Baadhi ya makazi ya jamii mjini Bukoba yaliyozingirwa na maji kufuatia kuongezeka kwa kina cha maji katika ziwa Victoria

Kwa upande wake katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Eng Pasaka Bakari amesema kuwa baada ya mafuriko kutokea ofisi ya mbunge ilifika kwa waanga katika kata zote 7 zilizoathirika na mafuriko hayo  ili kuona athari zilizotokana na mafuriko hayo ambapo  amewashukuru  wadau   mbalimbali wa maendeleo katika Manispaa ya Bukoba wanaoendelea kuwasaidia waanga na kuwaomba wengine kuendelea  kujitokeza  kuwasaidia.

Amesema kuwa Mbunge wa Jimbo  la Bukoba mjini  Adv Stephen Byabato ataendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuona namna ya kuwasaidia waanga wa mafuriko.

Kwa upande wake Afisa tawala wilaya ya Bukoba mjini akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Bukoba Ajesy Katumwa amewashukuru wadau wa group la Bukoba mjini Mpya kwa ushirikiano wao na kuona umuhimu wa kutoa misaada hiyo kupitia michango yao.

Baadhi ya wanakikundi wakiwasilisha michango yao kwa waathirika wa mafuriko mjini Bukoba

Bwana Katumwa amesema kuwa mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo makazi ya wananchi kujaa maji,Barabara kufungwa kwa muda katika baadhi ya maeneo pamoja na wananchi kuharibikiwa na mali zao.

Nao wananchi waliopatiwa msaada huo wameshukuru wadau wa Group la Bukoba Mjini Mpya pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini   kwa msaada walioutoa kwani mvua hizo zilisomba vyakula pamoja na vitu vingine  na maji yamejaa kwenye nyumba zao hivyo  kuwahimiza wadau wengine kuendelea kutoa msaada kwani wahitaji ni wengi walioathiriwa na mafuriko hayo.

Mwandishi: Mariam Kagenda-Kagera

Post a Comment

0 Comments