Wakulima wa Mpunga Titye wanufaika

Wakulima zaidi ya 800 wa zao la mpunga katika skimu ya Titye iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamefanikiwa kuongeza uzalishaji kutoka gunia tano hadi gunia 31.5 kwa hekali moja

Akiongea kuhusu mafanikio ya skimu hiyo yenye hekta zaidi ya 700 mwenyekiti wa skimu  Daud Mubingo amesema wamefanikiwa kuongeza uzalishaji kwa kuzingatia maelekezo ya kilimo chenye tija kutoka kwa wataalamu wa kilimo wa Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Kihinga mkoani Kigoma ambao wamekuwa washikirikiana na wakulima katika kila hatua ya uzalishaji kupitia mashamba darasa.

“Tumefanikiwa kuongeza uzalishaji kwasababu tumeacha kilimo cha mazoea na kuingia katika kilimo bora kinachozingatia matumizi ya mbegu za kisasa, viuatilifu na matumizi ya pembejeo kwa wakati” Amesema Mubingo.


Mwenyekiti ametoa angalizo kwa wakulima kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo na kuwa yeyote atakayekiuka atatakiwa kulipa faini ya shilingi elfu 50,000/= kwa wakulima wa skimu ya Titye, na hii ni hamasa kuwa kila mkulima.

 

Akiongea changamoto Felix Lukeba mwenyekiti wa kijiji cha Titye ameoimba serikali  kuwaboreshea miundombinu ya mifereji ya umwagiliaji pamoja na barabara ili waweze kupunguza gharama za uzalishaji hasa katika usafirishaji wa mazao yao 


“Tulijenga madaraja ili kurahisisha usafirishaji, bahati mbaya mwaka huu mvua zimekuwa nyingi, barabara zimeharibika, tunaomba serikali itusaidie kwenye yale maeneo tuliyojenga madaraja watuunganishe na barabara ili tuweze kupita kwakuwa tunazunguka umbali mrefu kutafuta barabara inayopitika” Amesema Lukeba.


Baadhi ya mashamba ya mpunga katika bonde la umwagiliaji la mto Ruchugi lililopo kata ya Titye 


Naye Eliazar Mizigiro diwani wa kata hiyo ameiomba taasisi ya TARI kuendelea kutoa mbegu za kisasa za kilimo cha mpunga zinazohitajika kwa wakati ili kuongeza uzalishaji sambamba na mbolea zinazotosheleza mahitaji ili kufikia azma ya serikali ya kumtoa mkulima kwenye kilimo duni na kumuingiza kwenye kilimo chenye tija.


“Nia ya mabadiliko tunayo kwakuwa tumejionea kwa macho namna ambavyo uzalishaji kwa kutumia kilimo cha kisasa unavyomsaidia mkulima kutoka kwenye umaskini, naomba serikali kupitia TARI ituletee mbegu na mbolea kwa wakati, na maboresho ya miundombinu mengine ifanyiwe kazi kwa wakati kwaajili ya ustawi wa mkulima na taifa kwa ujumla” Alisema Mizigiro.


Mkulima Nicholous Kibadi amewataka wakulima wenzake kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo na hiyo inatokana na manufaa yatokanayo na ushauri huo kwani kwa upande wake amenufaika na kuongeza kipato, kusomesha watoto katika shule za watu binafsi pamoja na kubadili chakula kitu ambacho kilikuwa kigumu kwake kabla ya kuongeza uzalishaji.


Kwa upande wa mhandisi wa kilimo mkoani Kigoma Bathromeo Moris amesema serikali inaendelea kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na kwamba fedha za ukarabati wa miundombinu ya mifereji zitakuja kupitia tume ya umwagiliaji huku akiwasihi   kuzingatia usafi wa mifereji hiyo ili kuifanya kuwa endelevu. 


Akizungumza mkurugenzi wa TARI Kihinga mkoa wa Kigoma Filson Kagimbo alisema kilimo cha umwagiliji cha zao la mpunga mkoani humo ni matokeo ya mradi wa mapinduzi ya kilimo kupitia urutubishaji wa mazao ya nafaka Afrika (NUTCAT) na Taasisi ya kurubisha mimea afica (NPI) unaotekelezwa katika nchi 10 za Afrika katika mazao manne yakiwemo mahindi, mpunga na ngano kwa muda wa miaka mitatu kuanzia 2022/2024.


Kagimbo amesema mradi huo kwa Tanzania unaotekelezwa mkoani Kigoma katika wilaya za Kakonko, Kasulu na Kigoma ambapo mpaka sasa mradi huo umekuwa na tija kwa wakulima kuongeza uzalishaji.


Mkurugenzi wa TARI KIHINGA Filson Kagimbo akiwa na mgeni rasmi ambaye ni katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Theresia Mtewele katika hafla ya siku ya kilimo cha mpunga iliyofanyika katika kijiji cha Titye


Akizungumza na Buha news katibu tawala wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Theresia Mtewele alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la matumizi ya ardhi na ongezeko la watu linasababisha kupungua kwa rutuba kwenye ardhi na hivyo kupunguza uzalishaji hivyo nchi imejiwekea mikakati ya kuongeza uzalishaji


“Lengo la taifa kupitia ajenda ya 1030 ni kujitosheleza kwa chakula na kuwa ghala la chakula la Afrika ifikapo 2030 hivyo serikali imejikita katika kufanya utafiti, uboreshaji na uendeshaji wa miundombinu ya umwagiliaji upatikanaji rahisi wa pembejeo pamoja na huduma za ugani na tunaona namna ambavyo uzalishaji unaongezeka kufuatia mikakati hiyo’ Alisema Mtewele.


Alisema kwa takwimu za uzalishaji wa zao la mpunga kwa mwaka 2021 zao  hilo lilizalishwa mpaka kufikia tani milioni 2.6 na kwamba mpaka sasa zao hilo linazalishwa kwa zaidi ya tani milioni 3 kwa mwaka jambo ambalo linaonesha namna taifa  lilivyojikita katika usalama wa chakula.


Hata hivyo Mtewele alisema changamoto za mifereji na barabara zilizotolewa na wakulima zitafanyiwa kazi kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa kilimo na kwamba watawasiliana na mamlaka husika kama wakala wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) ili waweze kuunganisha barabara na madaraja yaliyojengwa na wananchi.


Metewele aliwataka kuendelea kukitunza chanzo cha maji ya mto Ruchugi ili watu wengi wazidi kunufaika na matumizi ya maji katika kilimo cha umwagiliji.


Bajeti ya kilimo kwa mwaka 2023/2024 imeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 970.8 kutoka shilingi bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023 ili  kuhakikisha leengo la taifa kupitia ajenda ya 1030 la kujitosheleza kwa chakula na kuwa ghala la chakula la Afrika ifikapo 2030 linafikwa.


Mwandishi: Adela Madyane.

Mhariri: Prosper Kwigize.

Post a Comment

0 Comments