Wizara ya habari yashukuru kupata 100% ya bajeti yake 2023/2024

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amesema baada ya Serikali kuipatia fedha zote za miradi ya Maendeleo zilizoombwa, Wizara imefanikiwa kutekeleza mipango yote iliyopangwa kutekelezwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amebainisha hayo tarehe 16 Mei, 2024 Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2024/ 2025. 

Waziri Nape ametaja mafanikio hayo ni pamoja na kuanzisha Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, iliyozinduliwa 3 Aprili, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema, sekta hiyo imefanikiwa pia kukamilisha kuhamishia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), shughuli zote za ujenzi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Kuhifadhi Data (NIDC).

"Tumefanikiwa kufanya tathmini ya hali ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016, na Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya Simu ya mwaka 1997, kuandaa Rasimu ya Sera Mpya ya Taifa ya TEHAMA ya 2024, itakayojumuisha, pamoja na mambo mengine, masuala ya Kampuni changa za TEHAMA (Startups)," amesema Waziri Nape. 

Amesema, wizara imekamilisha ujenzi wa Kilomita 3,008 na vituo 66 vya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kukamilisha Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) jijini Arusha, lililozinduliwa rasmi tarehe 2 Septemba, 2023 na Rais Samia.

Waziri Nape ametaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilisha ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) jijini Dodoma, lililozinduliwa rasmi Aprili 25, 2024 na Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema, sekta pia imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa miradi ya upanuzi wa usikivu wa redio za TBC katika maeneo 7 ya Serengeti-Mara, Bariadi-Simiyu, Ileje-Songwe, Njombe, Kilwa-Lindi, Unguja na Pemba, kukamilika, kuridhiwa na kuanza kutumika kwa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali 2024-2034 na miongozo sita ya Usimamizi wa Sekta ya TEHAMA.

"Sekta imefanikiwa kukamilisha majadiliano kati ya Serikali na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano (Consortium) kulikowezesha Serikali kulipwa Dola za Marekani milioni 33, kusainiwa kwa mikataba ya mauzo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi za Uganda wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 28.8, Malawi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5, na Kampuni ya Airtel wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.8," amesema. 

Amesema, pia sekta imefanikiwa kuunda Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Setelaiti nchini kwa ajili ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza shughuli za anga za juu nchini, kuanza ujenzi wa Makao Makuu ya TBC katika eneo la Vikonje jijini Dodoma, uliofikia asilimia 18, hadi Aprili, 2024, na kuanza ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya kufunga mitambo mipya ya kisasa ya uchapaji, uliofikia asilimia 35.

Post a Comment

0 Comments