Kasulu DC yapania kuinua ari ya vijana kwenye michezo


💢Halmashauri yaanza uwekezaji kwenye michezo shuleni


Wanafunzi washiriki wa Umoja wa Michezo Sekondari Tanzania (UMISETA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu wametakiwa kuwa na nidhamu na kujituma muda wote wawapo kambini ili waweze kupata matokeo mazuri katika michezo hiyo.

Kauli hiyo imetolewa Jumamosi Juni 1, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Semistatus Mashimba wakati anafungua mashindano hayo na kuwataka wasishiriki mashindano husika kwa mazoea bali wafanye mbinu ili kuibuka na ushindi.

 Amesema kuwa kwa kufanya hivyo itawasaidia washiriki hao kuweza kushinda katika mashindano ya UMISETA kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa na kuwaahidi kuwa iwapo watafanikiwa kufanya hivyo ataipa kipaumbele sekta ya michezo katika halmashauri anayoiongoza. 

Aidha, Dkt. Mashimba amewataka watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha afya na usalama wa wanamichezo unakua vyema wakati wote wawapo kambini kuanzia siku ya ufunguzi hadi kambi yao itakapovyunjwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Dkt. Semistatus H. Mashimba akijiandaa kurusha tufe kuashiria uzinduzi wa mashindano ya UMISETA. Picha na. Idara ya Habari Kasulu DC


"Nitoe shime kwa Afisa Mtendaji wa Kata na Kijiji tuhakikishe walimu na watoto hawa wako salama na mawasiliano yanakuwepo ili tuhakikishe tunaanza na kumaliza mashindano yetu salama", amesema.

Naye Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri hiyo, Iyogo Isuja amesema uwepo wa UMISETA mashuleni si upotezaji wa muda ila inawapa nafasi nzuri wanafunzi ambao ni washiriki wa michezo hiyo kuweza kufanya vizuri katika masomo pia.

Ambapo ameongeza kuwa kwa kushiriki michezo hiyo inawapa nafasi nzuri washiriki kujenga afya na akili zao kuwa vizuri pamoja na kuwa na fursa nzuri katika soko la ajira nchini.

Timu ya mpira wa mkono ya watoto wa kike na kiume pamoja na wakufunzi wao ikipita mbele mgeni rasmi ambae ni Mkurugenzi Mtendaji. Picha na. Twisile Nganga

Kwa upande wake Afisa Michezo na Utamaduni wa Halmashauri hiyo, Thomas Kisaka amesema matumaini ni makubwa ya kushinda michezo hiyo kwa ngazi zote watakazoshiriki kutokana na maandalizi mazuri waliyotoa walimu wa michezo waliokuwa nao.

Mwandishi. Twisile Nganga
Mhariri. Prosper Kwigize

Post a Comment

0 Comments