Kukithiri kwa Ukahaba wanafunzi vyuo vikuu ni janga kwa taifa

    

Wakati Tanzania ikiungana na mataifa yote duniani kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu mbalimbali wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati katika miji mikubwa wanatajwa kuwa katika hatari kubwa za kufanya au kufanyiwa ukatili kutokana na tamaa zinazowaingiza katika biashara za ngono.

Uchunguzi wa kikosi maalumu cha waandishi wa Habari umebaini kuwa Biashara ya ukahaba ni moja ya biashara zilizowahi kutokea katika miaka ya nyuma na zinaendelea kuwepo katika jamii na maisha ya watu, huku ikitajwa kua moja kati ya kitega uchumi miongoni mwa wanawake waasio na maadili.

Tanzania ni moja kati ya nchi isiyoruhusu biashara hiyo ikiwa ni kinyume cha sheria zilizowekwa,huku adhabu mbalimbali zikiwekwa kwa wahusika.

Licha ya Serikali kuweka sheria kali kudhibiti vitendo vinavyokiuka maadili, biashara hiyo imekua ikiendelea, Jiji la Dar es Salaam likitajwa kuongoza huku wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wakitajwa kua wahusika wa biashara hiyo.

Makala hii ya kiuchunguzi, itaangazia namna gani wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wanavyojihusisha na biashara hiyo.

Ukahaba miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu limekua tatizo linaloikumba Tanzania kwa sasa, huku wanafunzi wengi wakijikuta kukabiliwa na tamaa na changamoto za kifedha na baadhi yao wakigeukia ukahaba kama njia ya kujipatia kipato kwa haraka na kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Hali hii inaibua maswali mengi kuhusu sababu ya tatizo hilo, athari zake, na nini kifanyike kukabiliana nalo.

Uchunguzi uliofanywa na wanafunzi wa uandishi wa Habari kutoka shule kuu ya uandishi wa Habari na mawasiliano kwa umma SJMC katika vyuo mbalimbali nchini umebaini kuwepo kwa wanafunzi wanaojihusisha na biashara hiyo.

Aidha uchunguzi umebaini maeneo wanayofanyia biashara yakiwemo Riverside,Kitambaa cheupe, Dansa club, Juliana Liquid club, Ancle’s Mikocheni na Royal tour (Samora ),huku wanafunzi kuanzia miaka 20 na kuendelea wakihusika na biashara hiyo.

Ni majira ya saa 10 jioni timu ya uchunguzi ya waandishi kutoka SJMC wanafika katika maeneo ya sinza A na kuzungumza na moja ya mwanafunzi (kiume) ambaye amekua mteja wa wanafunzi wa kike wanaofanya biashara hiyo.

Baadhi ya wasichana kutoka mojawapo ya Vyuo Vikuu jijini Dar es Salaam waliokutwa katika moja ya kambi za siri kwa ajili ya kufanya biashara za ngono

Shesiki Gonga (si jina halisi) umri miaka 23 kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam mkazi wa Sinza A ambaye ni mpangaji katika nyumba maarufu ya mama T  amesema amekua akishuhudia wanafunzi wengi kutoka chuo hicho wakifanya biashara hiyo katika maeneo mbalimbali tajwa naye akiwa mtumiaji "Mteja" mkubwa wa wasichana hao.

“Nimeanza kutumia wadada wanaojiuza tangu mwaka wa pili chuoni wakati wa weekend mimi na marafiki zangu tukawa tunatembelea maeneo mbalimbali ya club pamoja na disco tukawa tunawaona  tunazangumza nao kuhusiana na maswala ya mapenzi wakawa wanakubali, mkikubaliana unamchukua” alisema Gonga

Gonga anaweka bayana kuwa kuwa baadhi ya wasichana  waosoma nae darasa moja hukimbia na kujificha pindi wanapogundua ni yeye.

‘’Nimekua niakikutana nao sana wanafunzi tunao soma nao, wamekua wakiona aibu na kukimbia kujificha wanapojua ni mimi” amesema.

Baada ya mahojiano na Gonga kukamilika ikalazimu timu ya waandishi kutembelea maeneo tajwa ili kujionea kinachoendelea huko.

Ni muda wa saa mbili na dakika 15 usiku, maeneo ya Sinza, clabu maarufu ya Kitambaa Cheupe, timu ya waandishi inajionea kundi kubwa la wasichana wakicheza muziki na wengine wakipata vinywaji, huku wengi wao wakivalia nguo za nusu utupu.

Waandishi wakabahatika kufanya mazungumzo na moja ya kijana aliyekuwa katika eneo hilo (jina limehifadhiwa) amesema ni ngumu kutambua yupi ni mwanafunzi na nani siyo kulingana na matendo yanayofanyika pale.

“Hapa wanakuja mabinti mbalimbali kama mnavyowaona inakua ngumu kuwatambua wanafunzi,kwa sababu wote wanakunywa pombe,nguo walizovaa ndio hizo unazoziona asilimia kubwa miili yao iko nje.” alisema

Aidha aliendelea kwa kusema kua nje ya kupata burudani ya muziki na vinywaji kumekua na biashara ya ukahaba nyuma ya pazia ikiendelea.

 “Wengi wanafanya biashara hapa kwa kujificha na kuigiza kama ni wateja wa kawaida hali inayofanya siyo rahisi kugundulika na watu, lakini unapowasogelea na kuzungumza nao kibiashara hufunguka na kuweka wazi”. alisema

Waandishi hawakuishia hapo, siku nyingine muda wa saa 12 jioni, inafika katika maeneo ya chuo cha uhasibu (IFM), na kuzungumza na baadhi ya wanafunzi kutaka kujua sababu na ukweli wa jambo hilo miongoni mwao.

Yunusi mohamedi Issa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho, shahada ya Science and Economic Finance amesema Maisha yamekua magumu hivyo inawalazimu wasichana hao kuingia katika biashara hiyo

 "Ni kweli wapo wanafunzi wanaofanya vitendo vya ukahaba tena wapo wengi sana, hasa kipindi ambacho Boom linachelewa kutoka au linapokuwa limeisha kutokana na kuwa wanafunzi wengi huwa na madeni wanayokopa wakati hawana pesa, hivyo pesa ya Boom inapoingia yote inaishia kwenye madeni."

Yunus ameongeza kuwa baadhi ya wanafunzi hubaki chuoni nyakati za usiku kwa kisingizio cha kufanya majadiliano kuhusu masomo, lakini huishia kufuatwa na watu wenye magari na kwenda wanapokujua.

Pia ameongezea kuwa wanafunzi wa chuo hicho wamekua wakifanya shughuri zao katika maeneo mbalimbali yakiwemo Pweza beach,Resort,club na Masaai Kinondoni.

 Aidha kwa upande wake amejitambulisha kwa jina moja la “J” wa Chuo cha Usafirishaji amesema amekua na marafiki ambao wanajihusisha na biashara hiyo.

“Marafiki zangu hao wanaishi maneo ya kigamboni wengi wao wanafanya shughuli hiyo kukidhi mahitaji yao kutokana na ugumu wa Maisha wanayoishi wamekua na madeni mengi” alisema

Timu ya waandishi kutoka SJMC ikafunga safari mpaka kwenye moja ha hosteli ya nje inayopatikana maeneo ya Mikocheni A wanayokaa wanafunzi wa vyuo mbalimbali kuzungumza na mlinzi wa hosteli hiyo kujua muda wanaotoka na kuingia wanafunzi hao hasa muda wa usiku na usafiri unaokuja kuwachukua.

‘’wasichana wamekua na tabia ya kutoka usiku bila kuaga, hata pia hawatoi taarifa,kuanzia muda wa saa tano ndo wanatoka saana wengi wao wakiondoka hurudi ahsubuhi na mapema na wanaorudi hurudi kuanzia saa nane za usiku,aah hapo nje ya geti hua nasikia saana milio ya pikipiki”, amesema Mzee Mussa mlinzi wa hosteli ya wanafunzi inayopatikana Mikocheni.A

Kasheshe Kipanga (Jina limefichwa) ni mlinzi katika hosteli zinazopatikana maeneo ya ubungo, alipoulizwa kuhusiana na swala la kutoka kwa wanafunzi hususani majira ya usiku, amesema

 "Wanafunzi wengi wana kawaida hiyo ya kutoka usiku japo siwezi kujua wanaenda wapi na kufanya nini ila walio wengi wanapenda kwenda kwenye kumbi za starehe hasa siku ambazo wanakua hawana vipindi "

Aliongezea kwa kusema mara nyingi wanaondoka kwa usafiri wa bodaboda, bajaji na wengine magari, maarufu kama Bolt.

Kufuatia hali hiyo waandishi wakazungumza na madereva wa pikipiki almaarufu bodaboda na bajaji walio karibu na maeneo a vyuo na hosteli kutaka kujua ni maeneo gani hasa huwapeleka wanafunzi hao nyakati hizo za usiku.

Benjamini Balainga ni dereva bodaboda kutoka Barakuda  amesema amewahi kuwapakia kuwapeleka maeneo mbalimbali nyakati hizo.

“Ninawabeba ndio na mara nyingi nawapeleka Club mbalimbali zikiwemo Leaders club, pia na hapo Sinza kama unaelekea Makumbusho, jina la hilo eneo silifahamu na nikuanzia saa tatu usiku” amesema Benjamini.

Kwa upande wake Emanueli Mwalongo dereva bajaji kutoka Ubungo amesema wateja wake wakubwa ni wanawake hasa wakati wa usiku.

“Maeneo ninayowapeleka ni Riverside, Landmark, Sinza King park lounge na BNB lodge na mara nyingi wamekua wasichana wadogo nikikadiria umri wao ni kama miaka 20 hivi”. amesema Mwalongo

Aidha Isihaka Omary dereva bodaboda kutoka Kariakoo amesema mara nyingi wamekua wakitumia mfumo wa Bolt kuwapeleka maeneo mbalimbali

“Wakati wa weekend, wanawake ndio nimekua nikibeba sana na kuwapeleka baa na wengine wako mtandaoni “wanarikwestiwa” unaenda unawabeba unawapeleka wengi ni mabinti kuanzia wa miaka ya 2000. amesema Omary.

Baadhi ya wasichana (wanafunzi) waliokutwa katika moja ya nyumba maalumu wakitumia vilevi mbalimbali ikiwemo pombe kali na uvutaji wa sigara ikiwemo SHISHA ambayo hutajwa kuwa na machara makubwa au huchanganywa na madawa ya kulevya.

Matumizi ya Madawa ya kulevya na ulevi wa kupindukia unatajwa kuwa ndiyo nyezo wanayotumia wasichana hao kuondoa aibu wakati wanapotekeleza jukumu hilo la kuuza miili yao kupitia vitendo vya ngono, huku baadhi ya wanaume hutumia njia hiyo kuwalewesha ili wawapate kiurahisi bila kulazimika kulipa pesa kwa ajili ya ngono.

Wengi wa wanafunzi wanatajwa kujihami na madhara ya kile wanachokiita ajali kazini hususani magonjwa ya ngono, na mimba, hivyo hulazimika kutumia madawa mbalimbali kuzuia uwezekano wa kupata mimba au magonjwa.  

Timu ya waandishi ikatembelea baadhi ya maduka dawa za binadamu yaliyo karibu na maeneo ya chuo kutaka kujua wateja wakubwa maeneo hayo na dawa zipi hasa hununuliwa kwa wingi

Muuzaji wa duka la dawa lililopo maeneo ya ubungo njiapanda ya chuo jina (limehifadhiwa) alipoulizwa kuhusiana na aina ya wateja anaowauzia dawa  amesema

"wateja wangu ni watu wa aina tofati kama unavyoona kwasababu dula liko maeneo ya barabarani na sehemu yenye mzunguko mkubwa wa watu hivyo watu tofauti tofauti huja kununua japo wengi ni wanafunzi wa chuo ambao zaidi wapo maeneo haya"

Aidha alipoulizwa kuhusiana na dawa ambazo wateja wake ni wanafunzi wa chuo hususani jinsia ya kike wanazokuja kununua amesema huwauzia dawa za kawaida ambazo yeye kama mmiliki wa duka la dawa amehalalishwa kuuza, lakini aliongezea kwa kusema lipo kundi kubwa linalokuja kutafuta dawa hatarishi kama dawa za utoaji mimba na dawa za kuzuia mimba hususani P2, nk ambazo yeye haziuzi kutokana na kwamba zilizo nyingi haziruhusiwi kisheria na ni hatarishi kwa afya ya binaadamu.

Februari 6, 2024, jijini Dar es Salaam Waziri wa Afya Mh. Waziri Ummy Mwalimu wakati akifungua mkutano wa siku Mbili wa mapitio ya kimkakati wa PEPFAR COP muhula wa 23 kwa lengo la kutathmini hatua iliyofikiwa kuhusu mwitikio wa VVU katika kufikia udhibiti wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 alihimiza jamii kuzingatia kanuni za afya na kuepuka kuingia katika vitendo hatarishi.

“Hata hivyo tunatambua kwamba kuna misuse ya hizi dawa hasa kwa watoto wa Shule ambao kwa sasa inaonekana wanaogopa zaidi mimba kuliko UKIMWI! Matumizi holela ya P2 yanaweza kuzalisha matatizo mengine makubwa ya kiafya kwa wasichana/wanawake. Wataalam wetu wamenihakikishia kuwa matumizi holela na ya mara kwa mara ya P2 yanaweza kusababisha ugumba na saratani.

Tunaendelea kuliangalia suala hili kwa mapana yake wakati tunaendelea kulijadili ndani ya Serikali na wadau, hatua ya haraka tutakazo kuchukua ni kuongeza kasi ya utoaji elimu ya juu ya madhara ya matumizi holela ya dawa hizi (P2). Nimeshawaelekeza timu yangu kulitekeleza hili haraka.” amasema Waziri wa Afya  Ummy Mwalimu

Benedict Nkwao ambaye ni Afisa Uhusiano Tasisi ya Ustawi wa Jamii alipoulizwa kuhusu taarifa za biashara ya ukahaba miongoni mwa wanafunzi  katika vyuo alisema hana cha kusema kwa sasa kwa sababu hana Ushahidi kuhusiana na taarifa hizo na kusema masuala hayo yanautaratibu wake pia katika kuyazungumzia

Katika kuendelea kuzungumza na uongozi wa vyuo vingine hawakuonesha ushirikiano katika jambo hilo.

Hivi karibuni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala amebainisha mbinu iliyopo ya kuondoa biashara hiyo katika Jiji la Dar es Salaam ikiwemo kutoa mitaji ya biashara kwa wahusika ili wakidhi mahitaji yao na kuachana na biashara ya ngono.

“Kwa hiyo tumeshaanza mikakati maalumu kuhakikisha angalau wengine tunawachukua wale ambao wako tayari na kuwapa fedha kidogo ili wawe na mitaji yao binafsi” amesema Albert Chalamila.

Moja ya hatari zinazowakabiri wanawake na wasichana wanaofanya biashara za ngono ni uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ikiwemo UKIMWI, kushambuliwa na makundi ya uhalifu, kuingia katika uraibu wa madawa ya kulevya ikiwemo uvutaji wa bangi.

Pamoja na athari za kisaikolojia wasichana wanaojihusisha na ukahaba wako katika hatari kubwa ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja sambamba na kuingiliwa kinyume na maumbile mambo ambayo yanadhalilisha utu na kuongeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Wizara ya Afya chini ya Waziri Ummy Mwalimu imeonesha takwimu ya maambukizi ya ukimwi kupungua kutoka wa asilimia 7 mwaka 2003/2004 hadi kufikia asilimia 4.4 mwaka 2022/2023, kukiwa na tofauti kati ya watu na maeneo mbalimbali ya kijiografia.

Aidha, Waziri Ummy anasema kupaumbele katika masuala ya VVU/UKIMWI ni pamoja na kulinda mafanikio yaliyopatikana, kupunguza maambukizi mapya hususani kwa vijana walio katika umri wa balehe pamoja na kupunguza maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

VIFUNGU VYA SHERIA.

Mahala pa kuhifadhi makahaba.

Sheria No. 49 ya 1962 s. 3 176A. Mtu yeyote akiwa ni muuza kilabu ya pombe, hoteli, nyumba, duka, chumba au mahali pengine panapofikiwa na watu mara kwa mara kwa ajili ya kununua au kunywa viburudisho vya namna yoyote, anayeruhusu au kukubali kwa makusudi makahaba wa kawaida kukusanyika na kubaki katika jengo lake kwa ajili ya ukahaba, mtu huyo atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atawajibika kwa adhabu ya faini isiyozidi shilingi mia tano au, iwapo ni kosa la mara ya pili na kuendelea atatozwa faini isiyozidi shilingi elfu moja

Wavivu na wazembe.

Sheria Nos 49 ya 1962; 11 ya 1983 Jedwal176 Mtu yeyote kati ya watu wafuatao:- (a) Malaya mzoefu atakayefanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara au kuzurura au kushawishi mahali popote pa hadhara kwa ajili ya kufanya umalayaatahesabiwa kuwa ni mtu mvivu na mzembe na atapaswa kulipwa faini isiyozidi shilingi mia tano au kifungo kisichozidi miezi mitatu au vyote kwa pamoja.

KUHUSU KAULI YA MWANA SAIKOLOJIA

‘’Ni jambo ambalo linaweza kumletea msongo wa Mawazo (anxiety)  kwa kuhisi mambo mbali mbali ikiwemo kuwa na wasi wasi  labda kuhusu kutambuliwa na marafiki wake,familia au hata wanafunzi wenzake chuoni, na vilevile pia kua na msongo wa Mawazo namna ambavyo kama tunavyoona wanavyokatatwa na polisi na hata adhari za kiafya  kama magonjwa ya zinaa.

Na tunaona pia athari nyingine kama Hatari ya Kukosa Mafanikio Kimasomo, wasiwasi, na matatizo mengine ya kiakili yanaweza kuathiri utendaji wake darasani na kusababisha kushuka kwa viwango vya masomo”. Amesema Mwanasaikologia Elias Lukata Kutoka tasisi ya TUSPO

KUHUSU KAULI YA DAKTARI

“Kufanya ngono mara nyingi kwa kipindi kifupi kunaweza kusababisha maumivu au uchungu kwenye maeneo ya siri kutokana na msuguano na kuleta mchubuko  jambo ambalo linaweza kuleta adhari zaidi ya kupata magonjwa ya kuambukiza ikiwemo ukimwi,kisonono na vilevile maambukizi ya bakteria kama vile vaginosis ya bakteria na maambukizi ya fangasi, na hata hivyo Maambukizi ya mara kwa mara ya magonjwa ya zinaa yanaweza kuathiri mfumo wa uzazi wa mwanamke na kusababisha matatizo ya kupata mimba baadaye.”amesema dokta Mercy Mwanukuzi daktari kutoka hospitali ya KAIRUKI.

TUKIO LA KUKAMATWA KWA MADADA POA MAENEO YA SINZA.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko akiwa na Timu yake usiku wa June 15,2024 katika eneo la Sinza Jijini Dar es salaam wameendelea na oparesheni ya kushtukiza  kwa lengo la kuyabaini na kuyafungia maeneo yanayotumiwa na Madada poa kuuza miili yao (Madanguro) ambapo wamefanikisha kukamatwa Watu 30 wakiwemo Madada poa 25 pamoja na Wateja wao watano.


DC Bomboko amesema “Makaka poa na Madada poa, Mashoga na Wasagaji wote hawana nafasi katika Wilaya ya Ubungo na wote wanaofanya biashara hizi warudi wakafanye shughuli nyingine, naagiza hawa wote waende kituo cha Polisi na baada ya Sikukuu wapelekwe Mahakamani na nielekeze oparesheni iwe endelevu maeneo yote, Watendaji wa Mitaa na Kata, Maafisa Tarafa na Polisi Kata na wengine Mimi nawaonesha mfano wajibu wa kupambana na Makahaba ni wa kwetu sote”

KAULI ZA VIONGOZI WA DINI

Imamu wa Masjid Nuru Mleni Bakari Sarai amelizungumzia suala Hilo kuwa" Sheria ya kiislam inakataza kuuza miili na ni zinaa inayofanyika, Mungu amesema ni njia chafu nakuhusu watoto ni watoto hawana kosa ila watabaki watoto wamama kwasababu wamepatikana katika taratibu isiyo ya kisheria "

Pia ameongezea kuwa suala Hilo "Kiujumla nijambo lakulipiga vita mwisho litatuletea watoto mtaani"

Mchungaji wa kanisa la Grace Primitive Baptist church Kenny John Mwankenja amesema"Biblia ndio kitabi chenye utaratibu na kanuni kwenye agano la kale ilikuwa mtu akikamatwa anafanya ukahaba au kuzini ni wanapigwa mpaka kufa Ukahaba hauruhusiwi sababu dini zipo kusaidia kufuata taratibu Sheria na utamaduni, na ndoa za jinsia Moja hazitambuliwi ila ndoa ya mke na mume ndo Biblia zinazozitambua kwa wazazi wa pande zote mbili kulidhia na kanisa hutoa vyeti vya ndoa  kwaniaba ya Serikali na hakuna umri unaosema ndo unaruhusu kufanya biashara hizo".amesema mchungaji Kenny

KAULI ZA WANAFUNZI WAOFANYA BIASHARA CHUONI

Janeth John mwnafunzi wa stashahada ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano Kwa Umma kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na mawasiliano kwa Umma ni mjasiliamali wa nguo za ndani  na kiume pamoja na Matisheti amesema “nashukuru mungu biasharaaa inasaidiaaa ninapataa pesa ya kujikimu pia naepuka vishawishi na napenda kuwashauri wanafunzi wenzangu wanao Fanya biashara ya kuuza Miili yao waaache na kujiajiri wenyewe kwani biasharaaa inasaidiaaa sana”.

Mimi najishughulisha na biashara ya perfumes,nimeamua kufanya biashara hii kutokana na kujipatia kipato kulingana na maisha ya nyumbani kutokana mimi kama mtoto wakike kuna mahitaji huwa na hitaji kupata kutokana na hayo mahitaji yangu nikaamua kuanzisha biashara ili kuepusha vishawishi kutoka kwa wanaume na kutafuta pesa yangu mwenyewe sababu hakuna vitu vya bure”amesema  Sophia Daudi mwanafunzi kutoka SJMC.

KAULI YA VIONGOZI KUTOKA CHUO

Dr Edga Ngelela mkuu wa kitengo cha Mawasiliano ya Umma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano kwa Umma amesema

“kwanza  nikianza kuzungumza kihistoria suala kama hili la wanafunzi kujiuza limeanza tangu muda na wakati Fulani tulikua tukisikia Sinza mara wapi kule na maeneo mbalimbali  maeneo ambayo watu hujiuza,sasa kwa kuanza kuzunguza sitaki kuzungumza moja kwa moja kwa sababu ni mbaya kwa sababu kuna hali wanafunzi akikusimulia unabaki kua dilemma,unakuta mwanafunzi ametoka kwao hana hela amekuja kwenye hali ya kupata boom amepata asilimia 20 na hiyo asilimia 20 ana wadogo zake wanasoma kwa hiyo ajigawie yeye wadogo zake na wazazi nyumbani wanasema hela hakuna njia apekee anayogundua baadae kuifanya kwa sababu njia zingine zoote za kufanya ilia pate pesa zimegoma kwa hiyo anamuua kuona njia hiyo inamfaa,kwa maana nyingine amejitoa sadaka kwa familia yake,kwa hiyo ni moja wapo ya hali inayoweza kupelekea mwanafunzi kuingia katika hali hiyo”amesema Edga

Aidha ameongezea kwa kusema masuala ya kuathiriwa kisaikologia kutokana na vitendo walivyofanyiwa ikiwemo kubakwa na watuwao wa karibu imeka sababu ya wao kuathirika na kuendelea kufanya vitendo hivyo.

“Imefikia hata wengine hatua ya kutoweza hata kulala bila kulala na mwanaume kwa hiyo anaona njia nzuri ni Kwenda kujiuza”

Pia Dr Edga amesema kuna kundi lingine la wasichana ambao tamaa miongoni mwao imeka kishawishi kikubwa kwa wao kujihusisha.

“kwamba Fulani ana kile na kile unakuta nayeye anataka kua navyo kwa siku moja sasa hao nao wanaingia kwenye shughuli hiyohiyo wanataka na wakati angeweza kufanya njia nyingine ya maana ya kujikidhi”amesema Edga

Dr.Edga anaendelea kwa kutoa rai kwa wazazi kucheza kwa nafasi yao katika malezi bora ya Watoto wao .

Aidha amesema kama chuo amekua na kitengo maalumu cha kuwashauri wanafunzi ambao wamekua wakigungua wanapitia adha hiyo kwa kuwapa ushauri na hata msaada wa kifedha.

“Lakini kumekua na watu wengine wamekua na tabia tu ana kuona tu nisawa na kuona kumshauri ni kama umepitwa na wakati,kwahiyo hata kumshauri inakua ni ngumu sana na huyu anaendelea na tabia hizo.”amesema Edga.

KAULI YA MWENYKITI WA SERIKALI YA WANAFUNZI DARUSO SJMC

“Ni kweli Kuna baadhi ya tetesi zinazoonesha baadhi ya wanafunzi wanawake kujiuza, Mimi kama kiongzi kitendo cha wanafunzi kujiuza ni mmomonyoko wa maadili kwasababu wote tumekua Kwa lengo la kutafuta elimu na wazazi wetu wanatutegemea kwahiyo ukianza kujiingiza katika biashara hiyo kunaweza kusababisha kwa mwanafunzi kushuka kitaaluma na hata kupata magonjwa ambayo yatasabanisha kushindwa kufanya vizuri kitaaluma, Kwahiyo ninaomba wanafunzi wenzangu kuacha hii tabia ili tuweze kutimiza lengo la kuwa chuo na kuweza kuimarisha maisha yetu ya baadae kwaajili yetu na familia yetu ya baadae pamoja na kuwasaidia wazazi wetu” amesema Ramadhani Fupi.

KAULI YA MUHUSIKA

Anaitwa Loveness Chikawe mwanafunzi wa mwaka wa tatu kozi ya Doctar of Medicine (MD) kutoka chuo (kimehifadhiwa) amesema amekua akipitia changamoto nyingi hali iliyomlazimu kujiingiza katika kitendo hicho.

“Mimi nyumbani ndio wa kwanza kuzaliwa nimekua nikitegemewa nyumbani pia katika kuisaidia familia, nimeanza shughuri hii tangu mwaka wa pili mwanzoni hivi baada ya kuona Maisha yanakua magumu kwangu,boom ninalolipata limekua dogo kwangu halikidhi mahitaji yangu kwa ujumla.”

Alipoulizwa ni kwanini asingejikita katika biashara zingine kama wanafunzi wengine amesema”nilijaribu nilivyoingia tangu mwaka wa kwanza nilikua nikiuza ubuyu ,pipi kwa wanafunzi lakini bado haikuniletea faida kama nilivyotegemea kwa sababu hata Biashara ikawa inatumia muda mrefu kuisha ikapelekea kushindwa kuendelea kuimudu”

Alipoulizwa biashara yake huifanya vipi amesema “mimi tayari ninawateja zangu wenye mtandao kwa hiyo hua ninatafutwa kwa njia ya simu tu, na hua ni watu wazima kuanzia kama miaka 45 na kuendelea kwa sababu vijana wamekua na changamoto kubwa kwangu,unakuta mnakubaliana hela Fulani lakini ukifika kule mkimaliza anakupa hela ambayo hamjakubaliana lakini kwa watu wazima inakua ni tofauti kidogo.”

“Sijawahi kukutana na changamoto yoyote kubwa ambayo labda ingenifanya niache,ninapata hela kama unavyoona sasahivi niko kwenye chumba changu mwenyewe na kina kila kitu”amesema Loveness.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments