Mkurugenzi wa INEC aonya dhidi ya taarifa za upotoshaji.


Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), ,Ramadhani Kailima amewaonya waandishi wa habari, viongozi wa siasa wananchi na wadau wengine wa uchanguzi kuacha kutoa maneno ya upotoshaji kuhusu uhalali wa wajumbe wa tume hiyo kwani ipo kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Mkurugenzi ametoa onyo hilo baada ya mjumbe katika mkutano wa wadau wa uchaguzi wa mkoa Kigoma Sadick Bashangwe kuibua hoja ya kutaka wajumbe wa Tume ya Uchanguzi (NEC) kujiuzulu kwani tume hiyo haipo tena na sasa tuna Tume Huru ya Uchaguzi huku wajumbe na wakurugenzi wakibaki kuwa wale wale.

Amesema wajumbe wa tume hiyo wapo kisheria sawasawa na katiba ibara ya 5 (iii) na ibara ya 74 (vi) pamoja na sheria ya Tume Huru ya Uchanguzi ya mwaka 2024 na kwamba tume hiyo haitekelezi kazi yoyote ambayo haijapangwa na Bunge.

Pamoja na hilo Mkurugenzi huyo amewataka wadau wa siasa na viongozi wa dini kutumia majukwaa yao na nafasi zao kwenye jamii kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi la uboresha wa taarifa za mpiga kura.

Hata hivyo, INEC imewataka viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kufuata sheria,Kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa ili kuwasilisha malalamiko yao badala ya kufanya vurugu ambazo zitasababisha kuvuruga zoezi la uchaguzi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa INEC, Jacobs Mwambegele amesema Tume imejipanga kuhakikisha inashughulikia malalamiko yote ambayo yatapokelewa kutoka kwa wadau wote wa uchaguzi.

Amesema tume imefanya maboresho makubwa katika uboreshaji wa uandikishaji kwa mwaka huu kwani kutakuwa na matumizi ya kuboresha taarifa hizo kidigitali jambo ambalo litaokoa muda wa watu kukaa muda mrefu kituoni wakisubiri kuandikishwa kwani watu wataweza kuboresha taarifa zao kwa kutumia simu zao za mkononi na vifaa vingine walivyo navyo.

Wakitoa maoni baadhi ya washiriki katika mkutano huo, katibu wa chama cha ACT Wazalendo mkoa wa Kigoma, Yunus Luhonvya amesema kuwa ni muhimu Tume Huru ya uchaguzi kuangalia kipengele cha kulipa mawakala wakati wa zoezi la uboreshaji wa daftari na wakati wa upigaji kura kwani vyama vingi vya siasa havina uwezo wa kugharamia mawakala kutoka kwenye vyama vyao.

Mwandishi: Adela Madyane

Mhariri: Prosper Kwigize 

Post a Comment

0 Comments