Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia
wakimbizi UNHCR mkoani Kigoma, limeongoza maadhimisho ya siku ya kimataifa ya
mazingira maarufu kama Siku ya Mazingira duniani kwa kuhamasisha utunzaji wa
mazingira katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma
Maadhimisho hayo yamefanyika katika
Kambi ya wakimbizi mseto ya Nyarugusu wilayani Kasulu, wakati dunia
ikiadhimisha siku ya mazingira, mataifa mbalimbali yanakabiriwa na changamoto
nyingi za athari za mabadiliko ya tabia nchi hali inayopelekea uharibifu wa ardhi
na bayonuai kote ulimwenguni na kuamsha ari ya kila nchi kuweka mikakati ya
kupunguza athari hizo.
Akihutubia katika maadhimisho hayo
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isack Mwakisu ambaye alikuwa mgeni rasmi
ameweka bayana kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshuhudia uwepo wa
athari za kimazingira ikipoteza zaidi ya hekta 469,000 za misitu kila mwaka sambamba
na bayonuai mbalimbali
Kanali Mwakisu amebainisha kuwa ili kukabiliana na athari hizo juhudi za makusudi na za pamoja lazima zifanyike ikiwa ni pamoja na kupanda miti na kulinda vyanzo vya maji
Kwa upande wake mkuu wa ofisi ya shirika la
kuhudumia wakimbizi UNHCR wilayani Kasulu Bw. Jean Bosco Ngomoni amekiri kuwa shirika hilo linatambua uwepo wa
uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kuwahudumia wakimbizi katika
kambi zao na kwamba Umoja wa mataifa pamoja na wadau wake wanahakikisha kuwa
mazingira yanahifadhiwa na kurejeshwa katika uasili wake
Afisa mazingira wa UNHCR Bw. Godfrey
Oyema amebainisha kuwa Umoja wa unatambua umhimu wa kutunza mazingira, na
kwamba shughuli za upandaji miti zinapewa kipaumbele kwa kushirikisha jamii ya
wakimbizi na wenyeji.
“Tunaishukuru sana serikali ya
Ubelgiji, imetupatia pesa za kutosha kwa ajili ya mradi wa mazingira na madiliko
ya tabia nchi, na UNHCR kwa kushirikiana na wadau, wakimbizi na wenyeji tayari
tumeshapanda miti ipatayo milioni sita na kwa ujumla mazingira yako vizuri”
Amesisitiza Oyema.
Kaimu mkuu wa kambi ya wakimbizi
mseto ya Nyarugusu inayohifadhi raia wa Burundi na DRC Bw. Hamphrey Mrema
amekiri kuwa kutowapatia wakimbizi nishati mbadala ya kupikia ndiyo chanzo cha
uharibifu wa mazingira katika kambi hiyo huku akipongeza shirika la umoja wa
mataifa la kuhudumia wakimbizi kwa kutoa fedha kwa ajili ya kunusuru mazingira
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya
mazingira duniani mwaka huu ni “Ardhi yetu ndiyo kesho yetu.
Mwandishi: Prosper Kwigize
0 Comments