Tunzeni fedha vizuri ni gharama kuzichapisha


Benki kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kuheshimu na kuzitunza fedha za Tanzania vizuri kwani ni moja ya tunu za taifa.

Hayo yamesemwa na Nolasco Maluli meneja wa huduma za Kibenki na sarafu kutoka BoT Dodoma.

Amesema kutokuheshimu fedha, kuzirusha rusha na kuzitunza vibaya kunasababisha uchakavu wa fedha hizo na Kuzifanya zipunguze thamani yake katika matumizi.

Amesema ni vyema wananchi wakatambua kuwa fedha hizo zinatengenezwa kwa gharama kubwa hivyo wananchi wanajukumu la kuzitunza ili zidumu kwa muda mrefu.

“Kutunza fedha vizuri kunapunguza uwezekano wa fedha kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji, kwani nchi inaigia gharama nyingi za fedha za kigeni hususani Dola kuchapishia fedha nje ya nchi amesema Maluli.

Naye Matilda Luvinga meneja msaidizi wa Sarafu amesema ni kosa la jinai kudhihaki sarafu au noti za Tanzania.

Amesema kwa mujibu wa kifungu namba 332A cha kanuni ya adhabu kama ilivorejewa mwaka 2022 kifungu namba 35 ni kosa kudhihaki fedha na mtu atakayebainika kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

"Ni kosa kisheria kutumia fedha kama pambo katika sherehe za maharusi, pesa zisibanwe na Pini au zisikunjwe kunjwe wakati wa kutunza, badala yake zitunzwe vizuri katika pochi au sehemu ambayo haitasababisha pesa kuharibika" Amesema Luvinga.

Aidha Luvinga amesema onyo la kutunza fedha vizuri lilitolewa mwaka 2002 na BoT na mwaka 2021 waraka wa utekelezaji wa onyo hilo ulitolewa ili kuchukua hatua kwa yeyote anayechezea pesa au kuzitunza vibaya.

Hata hivyo sheria ya BoT ya mwaka 2006 kifungu cha 26 inatoa mamlaka kwa benki kuu pekee kuharibu na kutengeneza pesa ya Tanzania hivyo ni kosa la jinai kwa yeyote atakayebainika kuharibu pesa hizo.

Mwandishi: Adela Madyane

Mhariri: Prosper Kwigize 

Post a Comment

0 Comments