Vibali vya ujirani mwema vyachangia ongezeko la wahamiaji haramu

Kufuatia kuwepo kwa ongezeko kubwa la wahamiaji wanaoanzisha makazi na biashara nchini Tanzania bila vibali, Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Hamadi Masauni amelitaka Jeshi la Uhamiaji mkoani Kigoma  kuongeza mbinu za kukabiliana na tatizo la watu wanaoingia nchini kwa vibali halali vya ujirani mwema kisha kukiuka makubaliano na kuishi nchini kinyume cha sheria.

Akiwa mpakani wa Tanzania na Burundi eneo la Manyovu wilayani Buhigwe Waziri Masauni amesema haridhishwi na utendaji wa maeneo ya mipakani kutokana na raia wa Burundi kuingia nchini na kukaa bila kuwa na vibali na wengine kutozingatia muda wa kuisha kwa vibali vyao.


Amesema watu hao ndani ya nchi hii ni wengi kuliko wale ambao serikali imekuwa ikifanya taratibu za kuwarejesha nchini kwao jambo ambalo lisipochukuliwa hatua za haraka litachangia kuiweka nchi katika hatari za kiusalama.


Watu wanaingia kwa vibali vya ujirani mwema na hawatoki, tuna uhakika gani kama hawapewi vitambulisho vya Taifa na vya mpiga kura? tunajuaje kama ni watanzania au sio watanzania? tunajua watu hao wana nia gani na nchi yetu? Je tunajua wanafanya nini huko mtaani?  Aliuliza waziri Masauni 


Akisisitiza kuhusu ulinzi amelitaka jeshi hilo kuhakikisha linadhibiti uingiaji kiholela wa watu kutoka nchi Jirani na kuishi kinyume cha sheria kwa kuhakikisha watu hao wanatambuliwa na mamlaka kwa mujibu wa vibali walivyopewa pamoja na kuzingatiwa kwa muda watakaoishi nchini.

Mkuu wa wilaya ya Buhigwe kanali Ngayarina (kushoto) na akifafanua hatua ambazo zinagukuliwa na kamati ua usalama ya wilaya kudhibiti wahamiaji haramu katika mpaka wa manyovu. Kulia ni Afisa wa Uhamiaji kutoka jamhuri ya Burundi, wapili kushoto ni Mh. Mhandisi hamad masauni waziri wa mambo ya ndani ya nchi wa Tanzania na wa pili kulia ni ndg. Jamali tamimu mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma.


Kwa upande wake Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhamiaji mkoani Kigoma Novat Dawson alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema kuwa inasababishwa na ukosefu wa alama za usalama katika vibali vya ujirani mwema ambavyo vinatumika kusafiria.


Vibali vya ujirani mwema havina alama ya kiusalama ya kudhibiti wanaoingia na kutoka, hata ukiviwekwa kwenye  mfumo haviwezi kuingia kwakuwa ni karatasi ambayo mtu amebandika picha yake, anagongewa muhuli na kuandikiwa kwa mkono, ikiwa haya ndio makubaliano ya ujirani mwema” alisema Dawson.


Kamishna Dawson alisema atazungumza na mamlaka za nchini Burundi kwenye vikao vya ujirani mwema ili kutafuta namna sahihi ya kuboresha vibali hivyo na kuongeza udhibiti kwa kuweka baadhi ya alama za kiusalama katika vitambulisho hivyo ili kuendeleza azma ya ujirani mwema ya kufanya biashara za mipakani na kuimarisha  soko la Afrika Mashariki.


Alisema kwa mujibu wa sheria,  vibali vya ujirani mwema, vinaruhusiwa kudumu kwa muda wa siku 14 ndani ya nchi husika na kwenda ndani ya nchi kwa urefu wa kilomita 10 kwasababu za kibiashara lakini raia wa Burundi wamekuwa wakikiuka sheria hiyo na kwenda nje ya mkoa wa Kigoma katika baadhi ya mikoa kama Dodoma, Tabora, Dar-es-Salaam hadi Zanzibar kwa shughuli za kilimo na biashara.


Dawson amesema jitihada za kudhibiti raia hao wanaokiuka sheria na makubaliano ya ujirani mwema zinaendelea kwa kupitia doria za mashambani, kwenye vyombo vya usafiri na sehemu za biashara mbapo kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Machi - Mei 2024 wamekamata raia wa Burundi 1365  kati ya hao raia 1210 wamefikishwa mahakamani na wengine kurudishwa nchini mwao.


Uchunguzi uliofanywa na Buha News umebaini kuwa vijiji vya Kumsenga, Kibuye na Kagezi wilayani Kibondo, Kitanga, Herushingo wilayani Kasulu, Kilelema, kajana na Kitambuka na Mnanila wilayani Buhigwe, Ilagara, Sibwesa, Kalya wilayani Kigoma ni miongoni mwa milango mkuu ya kuingia kwa wahamiaji wasio na vibali na wenye vibari vya ujirani mwema ambao wanapoingia nchini hufanya biashara mbalimbali ikiwemo Ngono, ajira katika vilabu vya pombe hasa mjini Kasulu, Kigoma, Makere, Mvygwe, Kakonko na Kibondo.


Vilabu vingi vya pombe mkoani Kigoma vimeajiri wasichana kutoka Bunrundi na licha ya kufahamika dhahiri kuwa si raia wa tanzania hakuna hatua zinazochukuliwa na imebainika kuwa baadhi yao walipenyeza hadi katika uandikishaji wa wapiga kura katika chaguzi zilizopita huku ikiaminika kuwa wapo baadhi ya raia wa nchi jirani ambao wana namba na vitambulisho vya NIDA.


Aidha wahamiaji wengi hutumika kama nguvu kazi mashambani na kwenye uchungaji wa mifugo katika wilaya za Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ambapo hata hivyo huzoea mazingira na kuanzisha makazi ikiwemo kuoa au kuolewa,


Misitu ya Makere kusini na kaskazini, Ramsa ya Malagarasi, pori la akiba Ilunde, vijiji vya Kagera Nkanda, Mvinza, Mulyabibi, Chekenya, Kabulanzwiri na vingine ni miongoni mwa maficho ya wahamiaji ambao hutumika kama vibarua mashambani.


Mwandishi: Adela Madyane

Mhariri: Prosper Kwigize


Post a Comment

0 Comments