Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania kuhojiwa kwanini hawarejei


 Serikali za Tanzania na Burundi zimetangaza rasmi kuwa wakimbizi wa Burundi waishio nchini Tanzania hawana sababu ya kuendelea kubaki uhamishoni na badala yake wanalazimika kurudi nchini mwao.

Azimio hilo limetangazwa mjini Kigoma na Waziri wa mambo ya ndani ya nchini Tanzania Hamad Masauni aliyeambatana na katibu mkuu wa wizara ya mambo ya ndani ya Burundi baada ya kumalizika kwa kikao cha ndani kilichojadili kuwa hakuna sababu kwa wakimbizi wa Burundi kuendelea kususia kurejea nchini mwao. 

Bw. Masauni ameeleza kuwa serikali zote mbili zimeazimia kuwa kutokana na kusuasua kwa zoezi la kuwarejesha wakimbizi nchini Burundi, serikali ya Tanzania itaendesha zoezi la kuwahoji wakimbizi wote juu ya kwanini hawataki kurejea Burundi licha ya jumuiya ya kimataifa kuthibitisha kuwa nchi ya Burundi ina amani. 

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa azimio hilo, katibu mkuu wa Wizara ya mambo ya ndani ya Burundi ambaye pia anashughulikia masuala ya maendeleo ya jamii na usalama wa raia Bw. Theofil Ndarufaiye aliyemwakilisha Waziri wa mambo ya ndani anasema Burundi ni nchi huru na ina amani ya kutosha na shughuli za maendeleo zinaendelea hivyo hawaoni sababu ni kwanini raia wake wapatao laki moja na nusu ambao ni wakimbizi wasirejee makwao 

Aidha Bw. Ndarufatiye anapendekeza hatua za kufunga kambi za wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania kuanza kutekelezwa hatua kwa hatua huku akirejea maafikiano ya pande tatu katika vikao vilivyofanyika nchini Tanzania na Burundi yaliyobainisha kuwa Burundi iko salama

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kigoma kamishna jenerali mstaafu wa jeshi la zima moto Thobias Andengenye ameweka bayana kuwa hakuna haja kwa wakimbizi hao kuendelea kuishi kambini ambako stara na utu wao inashuka na badala yake waende nchini mwao kushiriki ujenzi wan chi yao 

Tanzania inahifadhi wakimbizi wa Burundi wapatao laki moja na nusu katika kambi mbili ambao licha ya kupewa fursa ya kurejea wakipewa misaada mbalimbali ya kiutu bado mwamko wao wengi kurejea Burundi ni mdogo

Mwandishi: Prosper Kwigize


 

Post a Comment

0 Comments