Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele (katikati) akizungumza
na waandishi wa habari leo tarehe 25 Julai, 2024 mkoani Geita. Kulia ni Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume, Bw. Kailima Ramadhan na kushoto ni Mjumbe wa Tume, Mhe.
Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omar.
*****
Na. Mwandishi Wetu, Geita Wananchi watakaofanya
udanganyifu ili wajiandikishe zaidi ya mara moja wanatenda kosa na wakibainika
wanaweza kufungwa jela kifungo kisichopungua miezi sita na kulipa faini. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele leo
tarehe 25 Julai, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani
Geita. “Ningependa kusisitiza kuhusu
suala la kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja, jambo hili ni kosa
la kisheria kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024,” amesema. Jaji Mwambegele amefafanua
kuwa kifungu hicho kinasema mtu yeyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara
moja atakuwa ametenda kosa la kisheria na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini
isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki
tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na
kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja. Katika hatua nyingine, Jaji
Mwambegele amesisitiza kuwa hakuna uwezekano wa mtu kujiandikishamara mbili na taarifa zake kusalia kwenye
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuwa kabla ya kutoa nakala ya mwisho, Tume
hulisafisha Daftari kwa kuwaondoa wapiga kura waliojiandikisha zaidi ya mara
moja. “Mara baada ya uandikishwaji
wa wapiga kura kukamilishwa, taarifa zote huingizwa kwenye mfumo wa AFIS
(Automated Finger Print Identification System) ambao huwaonesha wote
waliojiandikisha kwenye Daftari zaidi ya mara moja. Wapiga kura wa aina hii
hufutwa moja kwa moja kwenye vituo vyote na kuwabakisha kwenye kituo
alichojiandisha mara ya mwisho,” amesema. Ameongeza kuwa orodha ya
waliojiandikisha zaidi ya mara moja hupelekwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya
hatua za kisheria na kwamba Tume imefanya hivyo katika chaguzi za nyuma ambapo
katika uandikishaji uliofanyika mwaka 2015, Tume ilibaini jumla ya wapiga kura
52,078 waliojiandikisha zaidi ya mara moja ambapo orodha yao ilikabidhiwa kwa
Jeshi la Polisi tarehe 27 Agosti, 2015 kwa ajili ya hatua za kisheria. “Katika uboreshaji wa Daftari
wa mwaka 2020, Tume ilibaini majina ya watu 42,301 ambao walijiandikisha zaidi
ya mara moja na orodha hiyo ilikabidhiwa kwa vyombo vinavyohusika na makosa ya
kijinai,” amesema Jaji Mwambegele. Ameeleza kuwa baada ya
kukamilika kwa uchakataji wa Daftari, Tume huchapisha na kuweka wazi Daftari
hilo chini ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani, Na. 1 ya mwaka 2024 ambapo wananchi hulikagua. “Baada ya kukamilika kwa
uchapishaji wa mwisho wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, vyama vya siasa
hupewa nakala tepe (soft copy), haijawahi kutokea jina likajitokeza zaidi ya
mara moja. Hivyo, hakuna uwezekano wa mtu kuandikishwa zaidi ya mara moja na
kuweza kutumia nafasi hiyo kuwa kwenye vituo zaidi ya kimoja siku ya kupiga
kura,” amesema Jaji Mwambegele.
0 Comments