Balozi Dkt. Nchimbi atoa maagizo mazito TAMISEMI

Katibu mkuu wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt Emanuel Nchimbi amemwagiza Waziri wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kiasi cha shilingi milioni 200 zinapelekwa katika kituo cha afya Mwami Ntare Kasulu ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu itakayowezesha kufungwa kwa vifaa tiba ambavyo vimekosa sehemu ya kufanyiwa kazi

Agizo hilo amelitoa leo katika mkutano wa hadhara mjini Kasulu kufuatia ombi la Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini Profesa Joyce Ndalichako kuhusu kukwama kwa baadhi ya miundombinu katika kituo hicho kuipya kutokana na kuchelewa kwa pesa za ujenzi zilizoahidiwa na serikali.

Dkt. Nchimbi amebainisha kuwa itakuwa ni kutumia pesa za umma vibaya endapo vifaa tiba vilinunuliwa na kufikishawa katika kituo hicho cha afya kilichoko Kata ya Heru Juu Mjini Kasulu na kutofungwa kwa sababu ya kukosa jengo wakati serikali ilikwishatenga pesa kwa ajili hiyo.

Amemwagiza Naibu waziri wa TAMISEMI Zainab Katimba aliyekuwepo katika Mkutano huo kufikisha taarifa za agizo hilo kwa waziri Mchengerwa ili ahakikishe kiasi hicho cha pesa kinatumwa Kasulu.

"Ninakuagiza Naibu Waziri, uko hapa, mfikishia taarifa hizi Waziri na ahakikishe kabla ya mwisho wa mwaka huu ujenzi uwe umekamilika na vifaa tiba vianze kutumika ili kuwahudumia wananchi watakaokuwa na matatizo ya kiafya." Amesisitiza Balozi Dkt Nchimbi.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akipokea maelekezo ya Katibu mkuu wa CCM balozi Dkt. Emanuel Nchimbi ya kushughulikia na kutatua kero na malalamiko ya wananchi yaliyowasilishwa kwake wakati wa mkutano wa hadhara wa mjini Kasulu. Picha na Prosper Kwigize

Na katika hatua nyingine Katibu mkuu wa CCM balizi Dkt Nchimbi ametoa siku arobaini kwa waziri wa TAMISEMI kufika wilayani Kasulu kushughulikia tatizo la kusimamishwa udiwani kwa diwani wa Kata ya Kagerankanda kwa sababu za mgogoro wa uraia na kupelekea kata hiyo kukosa uwakilishi tangu mwaka 2021.

Akitoa agizo hilo Dkt. Nchimbi amebainisha kuwa TAMISEMI ndio wenye dhamana ya uongozi katika serikali za mitaa hivyo ni wazibu wa waziri kuhakikisha mgogoro huo unamalizika na wananchi wa kata ya Kagera Nkanda katika jimbo la Kasulu vijijini wanapata uwakilishi.

Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini Prof. Joyce Ndalichako akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa Katibu mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi, Ndalichako ametumia mkutano huo kumshukuru rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mamilioni ya fedha za miradi jimboni kwake. Picha na. Prosper Kwigize

Wakati huo huo Katibu mkuu wa CCM Balozi Nchimbi ameagiza Waziri wa Nishati ambaye pia ni naibu waziri Mkuu Dkt. Dotto Biteko kutatua kero ya kukatika kwa umeme kila wakati mjini Kasulu akitaja kuwa wananchi wanahaki ya kupata huduma tulivu ya umeme ili kujenga uchumi wao.

"Ninamwagiza Waziri wa Nishati kuhakikisha anafuatilia na kushughulikia kero ya kukatika umeme hapa Kasulu, haipaswi umeme ukatikekatike marakwa mara hii haifaki maana wananchi wanakosa huduma na wanashindwa kujenga uchumi wao" amesisitiza Balozi Dkt. Nchimbi.

Dkt Emanuel Nchimbi akifuatana na katibu wa itikadi na uenzezi taifa Comrade Amos Makala, katibu wa NEC oganaizesheni na katibu wa NEC mambo ya nje na maafisa wengine waandamizi wa CCM Makao makuu, wapo mkoani Kigoma kwa ajili ya ziara ya kikazi na kusikiliza kero za wananchi ambapo tayari zaidi ya kero 200 nyingi zikihusu migogoro ya ardhi zimerekodiwa na kukabidhiwa kwa mkuu wa mkoa ili azitatue.


Post a Comment

0 Comments