Hakuna mafanikio bila kufanya kazi kwa bidii-Dkt Samia

Kazi na sala, sala na kazi au asiyefanya kazi asile ni misemo maarufu inayotumiwa na viongozi wa dini na siasa tangu enzi na enzi. Nchi yenye wananchi wanaopenda kufanya kazi faida yake ni kuwa na shughuli nyingi za maendeleo na ubunifu katika shughuli hizo hali inayosaidia kukuza uchumi wake.

Akiongoza Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Julai 29, 2024 Ikulu jijini Dar es salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anasema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha biashara za mipakani na kuweka wepesi katika urasimishaji wa biashara hizo ili kuongeza chachu ya kukuza biashara na nchi jirani kupitia Jumuiya za Kikanda na Soko Huru Barani Afrika.

Huku akitaka utekelezaji wa azama hiyo ya Serikali isimamiwe na wakuu wa mikoa na wilaya za mipakani kwa kuondoa vikwazo na vizuizi visivyo vya lazima.

‘‘ Serikali itaendelea kuboresha mifumo ya usajili na taratibu za uwekezaji katika utekelezaji wa miradi ya ubia baina ya sekta ya umma na binafsi. Pia, itaunda kamati ambayo itashughulikia mfumo wa sera na sheria jinsi zinavyotekelezwa, ili kuondoa changamoto zilizopo kwa wafanyabiashara na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara nchini. Kamati hii itaundwa na wajumbe kutoka Serikalini na Sekta binafsi. ’’ Anabainisha Rais Samia

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko naye amesikika mara kadhaa akiwaasa Watanzania na hasa vijana juu ya umuhimu wa sala na kazi sambamba na kushiriki katika shughuli za ukuzaji uchumi na ushiriki wao katika miradi mbalimbali ya nchi.

Akizungumza katika Kongamano la Nne la Ushiriki wa Watanzania kwenye Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji nchini lililofanyika Aprili 29, 2024 jijini Dar es salaam, Dkt. Doto Biteko anawataka Watanzania kutumia fursa zilizopo kwenye uwekezaji miradi ya kimkakati kuhakikisha kuwa uwekezaji wanaoufanya unakuwa na tija kwa Watanzania na kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye kukuza uchumi.

‘‘ Mhe. Rais amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha uwepo wa sheria ya local content kusaidia kulinda watanzania wanaofanya biashara lakini nataka niwaase pamoja na kuwa na sheria hii muhimu jambo la msingi ni kuhakikisha mswahili mwenzetu anapopewa kazi tumuunge mkono, tushirikiane nae ili miradi ya ndani iweze kwenda mbele,’’ anasema Dkt. Biteko.

Anatolea mfano  kuwa awali  kampuni ikija kuwekeza nchini ilikuwa inaagiza kila kitu kutoka nje ya nchi na ndiomaana Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi limekuja na dhana ya local content ili kuipa nafasi nchi kuwa na nafasi kubwa ya biashara kufanywa nchini na kufanywa na watanzania wenyewe ili kukuza uchumi.

‘‘ Tufurahi kuona mswahili mwenzetu anapata kazi na kuifanya vizuri, tuwaunge mkono washirikiane ili miradi ya ndani iweze kwenda mbele na kuifanya kwa uaminifu na kupunguza maneno, pambana na rushwa kwenye michakato, badala ya kutumia fedha hizo kuhonga na kupunguza mtaji pindi unapopata kazi,’’ anasema Dkt. Biteko

Takwimu zinaonesha kuwa kwa sasa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo  mikubwa ya kandarasi takribani asilimia 97 ya miradi ya ndani imefanywa na watanzania.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi, Bengi Issa anamshukuru Rais kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kuongeza ajira, masoko na ushiriki wa Watanzania kwenye uwekezaji.

‘‘ Watanzania wanapokuwa wanafahamu miradi inayoendelea kwenye nchi yao, watakuwa na ufahamu wa namna ya kujipanga kupitia kampuni zao na kushiriki kwenye michakato ya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu kwenye utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya kiuchumi.’’ Anaeleza Bengi.

Ni dhahiri kuwa Serikali imekuwa na jitihada kadhaa za kuwezesha Watanzania kushiriki katika miradi ya kimkakati sambamba na kukuza uchumi wao kama mwananchi mmoja mmoja na wa Taifa kwa ujumla, hivyo ni jukumu la mfanyabiashara kufanya biashara kwa bidii ili kuongeza mapato yake, mkulima  alime kwa bidii na kwa kuzingatia kanuni za kilimo ili kupata mazao bora, mfanyakazi kufanya kazi kwa bidi na kwa matokeo sambamba na kazi yake ili kufikia mafanikio tarajiwa ya nchi.

Uchumi wa Tanzania ni himilivu, unaendelea kukua na kuimarika zaidi. Mwaka 2023 uchumi ulikua kwa 5.2% ukilinganishwa na 4.7% mwaka 2022. Hivyo kuendelea kuwa na uchumi imara kunachangizwa na wananchi kuendelea kufanyakazi kwa bidi.

Inaelezwa kuwa maeneo mengine yanayochochea ukuaji wa uchumi ni pamoja na uwepo wa uimara wa demokrasia ya uchumi ambapo milango ya masoko ya bidhaa nje ya nchi imefunguka, sambamba na nchi kuendelea kuvutia mitaji na uwekezaji kutoka nje.

 

Post a Comment

0 Comments