Homa hatari ya Nyani yatinga Burundi mamia wabainika

Watu wapatao 119 wamebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa homa itokanao na nyani (Mpox) wengine 483 wamekutwa na dalili za ugonjwa huo Nchini Burundi.

Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa afya nchini Burundi Mh. Baradahana Lydwine wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huo ambao umethibitishwa na shirika la afya duniani kuwa miongoni mwa magonjwa hatari ya kuambukiza.

Mh. Lydwine amebainisha kuwa serikali ya Burundi inaendelea na harakati za kuwapatia matibabu wagonjwa hao licha ya gharama zamatibabu kuwa kubwa ukilinganisha na uwezo wa uchumi wa raia wengi ambapo kutibu mgonjwa mmoja inagarimu kiasi cha Faranga1,000,000  pesa ya Burundi na kuongeza kuwa mgonjwa anamaliza kipindi cha wiki 3 akipewa matibabu hospitalini.

Idadi hio ya maambukizo ya ugonjwa huo inaripotiwa kuonekana katika maeneo 24 ya taifa la Burundi huku idadi kubwa zaidi ya maamukizi ikiripotiwa nchini jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 

Waziri amefahamisha kuwa mgonjwa wa MPOX anasafishwa kwa maji maalumu huku ikilazimika kufunikwa kama mtu alieungua moto, na vifaa vyote alivyolalia vinachomwa baadae na kwamba hii ndiyo sababu ya huduma kuwa ghali sana 

Aidha waziri wa afya amefahamisha kuwa serikali inafanya jitihada ya upatikanaji wa chanjo ambayo hata hivyo anataja kuwa huuzwa kwa dola nyingi na kwamba ni vema kuchukua tahadhali na kinga kuliko kutibiwa.

Amewataka watu wote kutilia maanani ugonjwa huo mkali na kusisitiza wananchi kufanya usafi kwa kiwango kikubwa kama ilivyofanwa wakati wa mlipuko wa CORONA.

Pamoja na mambo mengine inaelezwa kuwa ugonjwa wa homa ya Nyani unaosababisha mgonjwa kutokwa na upele na vidonda mwili mzima huambukizwa kwa njia ya kujamiana. 

Imeandikwa na. David NDEREYIMANA - Bujumbura

Post a Comment

0 Comments