Rais Dkt. Samia atoa maagizo mazito wizara ya Kilimo


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza

Wizara ya Kilimo kuisimamia kwa ukaribu Sekta ya Ushirika ili uwekezaji unaofanywa na

Serikali kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi uweze kufanywa na Vyama vya Ushirika.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo katika kikao na Maafisa Ugani na wanaushirika

kilichofanyika Ikulu, Chamwino.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Serikali ina dhamira ya kurudisha hadhi ya ushirika

hususan ushirika wa mazao hivyo ametaka Ushirika uendeshwe kisasa, uwekezaji ufanywe

kitaalam na ukiwa na lengo la kumnufaisha mwanaushirika moja kwa moja.

Vile vile, Rais Dkt. Samia amevitaka Vyama vya Ushirika kutokuwa sehemu ya kumyonya

mwanaushirika, bali viwe mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea.

Rais Dkt. Samia pia amevielekeza Vyama vya Ushirika kuwa chachu ya mabadiliko na

vyenye kuleta mageuzi ya fikra, ikiwemo kuchangia maendeleo mapana kwa kuhamasisha

wanaushirika waweze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na Mfuko wa Bima ya Afya kwa

wote.

Rais Dkt. Samia ameagiza Maafisa Ugani na Maafisa Ushirika kuhakikisha kuwa ruzuku ya

pembejeo inayotolewa na Serikali inaleta matokeo makubwa zaidi, kuwafikia wananchi vijijini

pamoja na kuwaelimisha mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kuandaa utaratibu wa

kuwapima Maafisa Ugani kwa tija inayozalishwa kwenye Kata au Kijiji anachokisimamia ili

uwekezaji unaoufanywa na Serikali utoe matokeo yanayotarajiwa.

Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia amewataka Maafisa Ugani katika ngazi ya Kata kukaa

kwenye vituo vyao na kutumia usafiri ambao Serikali imewapatia kuwafikia na kuwahudumia

wananchi.

Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali itaunga mkono juhudi za wanaushirika kuanzisha

Benki ya Ushirika ya Taifa kwa kuchangia Shilingi Bilioni 5 kama mtaji ili kuwezesha shughuli

za Benki hiyo kuanza.

Post a Comment

0 Comments