EWURA yawapa Onyo wafanya biashara wa Mafuta.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewaagiza wamiliki wote wa vituo vya mafuta ya Petroli nchini kuhakikisha wanachukua hatua stahiki zinazozingatia usalama wa Afya, mali na mazingira wakati wote wa uendeshaji wa  Biashara hizo.

Taarifa iliyotolewa Septemba 16, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, imewasisitiza wafanyabiashara ya vituo vya mafuta nchini kutoruhusu uuzwaji wa mafuta katika vifaa visivyoruhusiwa kuchukulia au kubebea mafuta ya petroli kama vile madumu, chupa aina zote na vifaa vingine visivyoruhusiwa kisheria.

"Tunawahimiza wamiliki wa vituo vya mafuta kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha ya watu, mali, na mazingira wakati wa uendeshaji wa biashara zao na kuchukua tahadhari stahiki kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 27 ya Kanuni zinasimamia biashara ya vituo vya mafuta nchini"Amesema Dkt. Andilile

EWURA imetoa agizo hilo kutokana na ongezeko la matukio ya milipuko ya moto inayotokana na uhifadhi au uuzaji holela wa mafuta ya petroli kwa kutumia madumu au chupa bila kuchukua  tahadhari za usalama wa Afya, mali na mazingira (HSE).

Pia, EWURA imebainisha kuwa, itaendelea kufanya ukaguzi wa kina kwenye vituo vya mafuta kote nchini ili kuhakikisha utekelezwaji wa kanuni hizo, na yeyote atakayekiuka hatua kali za kisheria ziatachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufungiwa kituo chake.

Kulingana na Taarifa iliyochapishwa na EWURA kulingana  na Kifungu cha 131 cha Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya mafuta sharti aombe na apate leseni kutoka EWURA. Kufanya biashara ya kuuza mafuta bila leseni ya EWURA adhabu yake ni faini ya shillingi million 20 au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.

Mwandisfhi; Ellukagha Kyusa

Post a Comment

0 Comments