Kalonzo Musyoka amkabiri Ruto uteuzi IEBC.

 

 

Kiongozi wa  Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka amemtaka Rais William Ruto kuharakisha mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akisema kutokuwepo kwa makamishna hao kunawanyima Wakenya haki ya uwakilishi.

Bw Musyoka alisema hayo Jumanne wakati wa Kongamano la Kitaifa lilokuwa likijadili Kuhusu Kukamilishwa kwa Mageuzi ya mfumo wa Uchaguzi kuelekea 2027 na kusisitiza kuwa ukosefu wa nia njema ya kisiasa unazuia utekelezaji wa sheria iliyoundwa Juni 2024 baada ya wabunge kupitisha Mswada wa marekebisho ya Sheria ya IEBC ya mwaka  2023.

Sheria hiyo inapendekeza kuundwa kwa jopo jipya la kuteua makamishna wa IEBC lenye wanachama tisa na hivyo kuharamisha uwepo wa jopo la zamani lenye wanachama saba liloongozwa na Kasisi Daktari Nelson Makanda.

“Inasikitisha kuwa IEBC bado haina makamishna watakaotekeleza mageuzi muhimu yanayohusiana na masuala ya uchaguzi, hamna nia ya kisiasa. Kuingiliwa kwa asasi za umma ndiko kumezuia kuwepo kwa tume halali itakayoweza kutekeleza majumu yake ya kikatiba,” Alisema Bw. Musyoka.

Bw. Musyoka ameongeza kuwa Majukumu muhimu ya IEBC ambayo yamekwama ni kama vile kufanyika kwa chaguzi ndogo katika maeneo  ya bunge na wadi kadhaa ambazo hazina wawakilishi pamoja na  uwekaji upya wa mipaka ya maeneo wakilishi na utayarishaji wa sera mbalimbali za kufanikisha utendaji kazi wa tume hiyo.

Kiongozi huyo wa Wiper pia alilaumu Jopo la Kutatua Mizozo inayohusiana na Vyama vya Kisiasa (PPDT) akisema imekosa kuzingatia kanuni ya usawa wa kijinsia katika uamuzi wake kuhusu uteuzi wa wanachama wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC.

 Bw Musyoka, alikuwa amewasilisha jina la Balozi Koki Muli kuchukua nafasi moja iliyotengewa muungano wa Azimio kati ya nafasi tatu zilizotengewa Kamati ya Ushirikishi wa Vyama vya Kisiasa (PPLC) katika jopo la kuteua makamishna wa IEBB.

                                          Aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC Wafula Chebukati. 

Kwa mujibu wa Gazeti la Taifa letu  mnamo tarehe 11 septemba 2024 , PPDT iliamua kuwa jina la Augustus Muli wa chama cha National Labour Party (NLP) ndio liwasilishwe na Azimio kama mwakilishi wake katika jopo hilo la watu tisa badala ya Balozi Koki Muli huku Asasi nyingine zinazotarajiwa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao katika jopo hilo ni Chama cha Mawakili Nchini (LSK), Baraza la Madhehebu Nchini (IRC), Chama cha Mahasibu Nchini (ICPAK) na Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Hata hivyo Majina hayo yote yanapaswa kuwasilishwa kwa tume ya PSC kisha yawasilishwe kwa Rais Ruto kwa uteuzi rasmi na  baada ya kuteuliwa rasmi  wanachama wa jopo hilo  litaapishwa na kuweka matangazo magazetini kuwaalika Wakenya waliohitimu kuwasilisha maombi ya kutaka kujaza nafasi ya mwenyekiti wa IEBC na makamishna sita.

IEBC ilisalia bila mwenyekiti na makamishna kuanzia Januari 17, 2023 baada  ya aliyekuwa mwenyekiti  wake Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu kukamilisha muda wao ,badae Desemba 2022 makamishna wengine watatu Juliana Cherera (Naibu Mwenyekiti) pamoja na Francis Wanderi na Justus Nyang’aya walilazimishwa kujiuzulu.

Mwandishi;Harieth Kamugisha

Mhariri;Ellukagha Kyusa


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments