Mahakama yakataa Ombi la Mpina kuongeza ushahidi wa Kesi

 


Mahakama Kuu ya Masijala jijini Dar es Salaam imetupilia  mbali ombi  la Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina  aliyeomba  Mahakama hiyo imruhusu awasilishe majibu ya nyongeza katika kesi ya kikatiba dhidi ya Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha pamoja na taasisi tano zikiwemo kampuni za vocha.

Mahakama imetoa uamuzi huo Septemba 18, 2024 kupitia kwa Jaji Arnold Kirekiano aliyesikiliza shauri hilo baada ya kukubaliana na mapingamizi yaliyowekwa na Serikali pamoja na wajibu maombi wengine walioomba Mahakama hiyo isitoe nafasi na isikubaliane na maombi ya Mpina.

Aidha kwa upande wa jopo la mawakili wa Mpina wakiongozwa na Dk Rugemereza Nshala ameomba mahakama iwape muda wa kupitia nyaraka za madai ya kesi hiyo kisha kuwasilisha majibu ya nyongeza ili kesi hiyo itakapofika muda wa kusikilizwa ushahidi uwe umekamilika.

Jaji Kirekiano amesema hawataruhusu watu wanaohitaji  kuleta maombi mengine mahakamani hapo, kwa ambao walikuwa wanaomba mahakama iwaruhusu wawasilishe majibu ya ziada baada ya kupokea majibu kwa wajibu maombi.

 Mpina amefungua shauri hilo la kikatiba namba 18383/2024 akipinga mambo kadhaa ikiwemo uamuzi wa Waziri wa Kilimo kutoa vibali vya ununuzi wa sukari kupitia Bodi ya Sukari kwa kampuni ambazo hazimiliki viwanda vya sukari .

Awali  kesi ya pili ni Mpina dhidi ya Waziri wa Kilimo Waziri wa Fedha, Kamshina wa TRA na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na kampuni ya Itel na Zanzibar Merchandise ambapo anahoji uhalali wa utaratibu uliotumika kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari ambapo Mpina anadai kuwa utaratibu huo ulikiuka Sheria, na  kuwa   vibali vinatakiwa kutolewa kwa muagizaji ambaye ni mzalishaji wa sukari.

Pia anapinga Waziri wa Fedha kuruhusu Kamisha wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuamuru kampuni za vocha kuingiza sukari nchini bila kulipa kodi na kupelekea Serikali kupoteza mapato ya zaidi ya Sh1.548 bilioni pia  amezishtaki kampuni za sukari kwa kukubali kuingiza sukari na kupewa msamaha wa kodi.


Mwandishi : Shukuruimana Revokatus

Mhariri:Abel Mahenge 

 

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments