Mradi wa tanki la maji Kibondo wafikia Asilimia 95

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko  amesema 2022/23 Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Kibondo ilitenga zaidi ya Shilingi Bilioni 1.49 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa tanki la maji lenye  ujazo wa lita 1,500,000 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 95.

Akizungumza Septemba 18, 2024 wilayani Kibondo mkoani Kigoma, mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tanki hilo, Dkt. Biteko amesema mradi huo unaojengwa na wataalam kwa kuwashirikisha vijana wa Kitanzania utasaidia kuounguza mgao na kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kwa siku na kuwataka  wananchi wa Kigoma kulinda vyanzo vya maji.

“Nataka niwaombe mnavyo vyanzo vya maji mvilinde, mkikata miti ovyo na kuchoma mashamba itasababisha ukame licha ya kuwa na tanki hili mvilinde vyanzo vya maji ili tupate maji kwa muda mrefu,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ametaja faida  za mradi huo kuwa ni kuboresha huduma ya maji kwa kuongeza saa za upatikanaji maji kutoka saa nne  za awali hadi 12 kwa siku, na kuwataka  wananchi wa Kigoma kushikamana na kujiepusha na migogoro na badala yake washirikiane ili kuendelea kujiletea maendeleo.

    Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko akizungumza na            wananchi wa Kibondo baada ya kutembelea mradi wa Tanki la maji. 

Awali  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya uendelezaji wa miradi na miundombinu ya maendeleo Mkoani Kigoma.

Amesema fedha hizo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuunda meli ambacho hakipo popote Afrika Mashariki na kati, Meli ya Mv Liemba ambayo tayari imetengewa fedha kwa ajili ya ukarabati na baada ya hapo itaendelea na safari zake kati ya Tanzania, Burundi na DRC Kongo.

“Tutaendelea kusimamia kila fedha ya miradi ambayo itaelekezwa mkoani kwetu kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Kigoma.” Amemalizia Mkuu huyo wa Mkoa.

Naye, Mbunge wa Kibondo Mjini, Mhe. Dkt. Florence Saminzi amesema kuwa Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika Jimbo la Muhambwe.

“Katika kipindi cha Rais Samia kumekuwa na maendeleo, tumepata shule tatu mpya za msingi pia tumeboresha madarasa, vyumba vya walimu pamoja na kupokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya,” amesema Dkt. Saminzi.

Mwandishi:Immaculate Makilika

Mhariri: Abel Mahenge 

Post a Comment

0 Comments