Rais Samia aelekeza rasilimali zinazochimbwa nchini ziwanufaishe Watanzania - DKT. Biteko


                   picha Wizara ya Nishati 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Watanzania kunufaika na rasilimali zinazochimbwa katika maeneo yao kwa kutoa fursa mbalimbali  ikiwemo  ajira.

 Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Septemba 10, 2024 mkoani Mtwara katika hafla ya kukabidhi leseni ya uendelezaji wa eneo la ugunduzi wa gesi asilia katika Kitalu cha Ruvuma, eneo la Ntorya ambapo Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) pamoja na Kampuni za ARA Petroleum Limited na Ndovu Resources Ltd ni wabia.

 “ Mhe. Rais alielekeza wananchi waliopo maeneo yenye rasilimali wanufaike kabla ya maeneo mengine, alitoa kibali cha mradi mkubwa wa gesi na tutajenga kiwanda cha kuzalisha gesi na kuboresha kituo cha kuzalisha umeme Songa.” Amesema Dkt. Biteko.

Dkt Biteko  amesema  katika mradi wa Ntorya vitachimbwa visima namba 1 na 2 pamoja na kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka katika kisima hadi Madimba kilomita 34 na katika kipindi cha miezi sita bomba litakuwa limejengwa. 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,katika Halfa ya kukabidhi  leseni ya uendelezaji wa Eneo la Ugunduzi wa Gesi la Ntorya .

 Biteko ameongeza kuwa, Madimba kuna vitongoji 18 na Msimbati  vitongoji 13 ambavyo  havina umeme vitakuwa  vimeunganishiwa umeme ifaikapo  mwezi Desemba, 2024, na  kwa upande wa  Songo Songo  vitongoji vyote  vitakuwa vimeunganishiwa  umeme ifikapa  tarehe 31 Oktoba, 2024.  Vilevile, Serikali  kupitia REA  inaendelea  na kazi ya kupeleka  umeme  katika vijiji 30 vya Mkoa wa Lindi ambapo  kazi hiyo  itakamilika ifikapo  mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2024.

 Aidha, katika kuhakikisha kuwa hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara inaendelea kuimarika, mnamo tarehe 31 Machi, 2024 Serikali ilikamilisha kufunga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa MW 20 , unaounganisha Mtwara na Lindi kupitia Tunduru .

 Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda amesema  kuwa matumizi ya gesi yamepungua kutokana  na ongezeko la umeme katika Gridi ya Taifa hivyo  gesi iliyokuwa inatumika kuzalisha  umeme itaelekezwa katika matumizi mengine, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya umeme uliokuwa unazalishwa awali  iiitokana na gesi.

 Balozi wa Omani nchini  Tanzania Mhe. Saud bin Hilal Alshaidani amesema kuwa tukio  la kukabidhi leseni ya kuendeleza kitalu hicho linaunganisha nchi za Tanzania na Oman na  itasaidia uchumi wa Tanzania.

 “ Tunatarajia katika ushirikiano  huu tutapata faida na kusaidia jamii ya Mtwara pamoja na kuitambulisha Tanzania huko duniani kama wazalishaji wa gesi,” ameeleza Balozi huyo.

Mkurugenzi wa  Shirika la Maendeleo ya Petroli  (TPDC), Bw. Musa Makame amesema kuwa mradi huo ulianza kwa kushirikiana kati ya Serikali, TPDC na Kampuni ya Ndovu Resources.

 “ Mwaka 2017 uchimbaji ulifanyika na kupata gesi, hadi sasa tuna futi trilioni 1.6 ambazo zimegundulika na kuhakikiwa, na mwaka huu hadi ujao tunachimba kisima na  tayari tuna visima viwili na tunaenda kuchimba cha tatu,” amesema Bw. Makame.

Ameongeza kuwa TPDC inajenga bomba la kusafirisha gesi  na kiwanda kidogo cha kuchakata gesi iwe kimiminika na kupeleka kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na mabomba na kisha kwenda kwenye maeneo mengine. ,Aidha, Shirika hilo litatoa fedha kiasi cha shilingi milioni 750 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya ikiwa ni sehemu ya faida ya uwepo wa mradi huo katika eneo hilo.

 

 Na Mwandishi wetu .


Post a Comment

0 Comments