Rais Samia amedhamiria kuufungua mkoa wa Kigoma- Biteko

 
📌Barabara ya Kakonko hadi Mpaka wa Burundi Kujengwa kwa Lami

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuipatia Kigoma miradi ya maendeleo na fursa mbalimbali ili kuufungua mkoa huo kiuchumi.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Kasanda Wilaya ya Kakonko leo Septemba 18, 2024 Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imetekeleza miradi mingi ya maendeleo mfano hospitali na barabara ikilinganishwa na kipindi kilichopita ambapo wananchi walikuwa kitaabika kupata huduma mbalimbali za kijamii.

 “ Halmashauri hii imeanzishwa mwaka 2013 na kwa kiasi kikubwa maeneo mengi yalikuwa mapori lakini leo tumetembelea Hospitali ya Wilaya ya Kakonko hali halisi ya maendeleo inaonekana, Rais wetu anataka Kigoma ifikike na watu wakae kwa amani na kufurahia kuwapo Kigoma, nimefurahi sana kuona majengo ya hospitali ya wilaya.” Amesema Dkt. Biteko.

Mh. Doto Biteko akiambatana na Naibu waziri wa TAMISEMI Mh. Zainab Katimba na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye wakati wakikagua Hospitali ya wilaya ya Kakonko.

Awali wananchi wa Kakonko walikuwa wakipata huduma za afya kutoka Hospitali ya Bugando na Geita, uwepo wa hospitali hiyo utasaidia kupunguza gharama ya kufuata  mbali huduma za afya.

 Akizungumzia barabara ya Kakonko hadi  mpaka wa Tanzania na Burundi  Dkt. Biteko amesema maisha ya watu ni kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita. "Hatutaki maigizo kwenye maisha ya watu, tunataka kuwahakikishia hata barabara ya Nyakanazi Kasulu  hadi Kigoma inaunganishwa kwa kiwango cha rami, Rais Samia anataka kuona tunafanya biashara na majirani zetu na kuwa mpakani sio laana bali ni fursa na milango ya biashara itafunguliwa na barabara hii yenye urefu wa km 48 ya Kakonko hadi mpakani itasimamiwa na TANROADS.” Amesema Dkt. Biteko.

 Vilevile, amewapongeza wananchi wa Kakonko kwa kuzalisha chakula cha ziada tani 81,000 ambapo mahitaji ni tani 76,000 na tani za chakula zilizopo ni tani 157,000.

Pamoja ya hayo, Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendesha mchakato mzuri wa kura za maoni na  wachague wagombea wenye sifa na sio kutumia rushwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainabu Katimba amesema kuwa Rais Samia amefanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni  4 kwa ajili ya majengo na vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, aidha ametoa maelekezo mahsusi kuwa hospitali zote za wilaya nchini  ziwe na wodi ya watoto ili kupunguza vifo kwa mama na mtoto.

Imebainishwa kuwa idadi ya Vifo vya watoto wachanga vimepungua  kutoka 556 hadi 104 katika vizazi hai 100,000.

Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada kubwa inayofanywa na Rais Samia kwa ajili ya akina mama nchini,” amesema Mhe. Katimba.

 Pia, Mhe. Katimba amezungumzia barabara na kusema kuwa  awali wilaya hiyo ilikuwa inapokea kiasi cha shilingi  milioni 700, katika kipindi cha Rais Samia ameongeza fedha hadi kufikia shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya barabara za dharura.

 “ Barabara inayoelekea hospitali ya wilaya yenye urefu wa km 1, mwaka huu Mhe.  Rais ametoa fedha shilingi milioni 450 ili iweze kujengwa na muweze kufika hospitali vizuri, hakika wilaya hii imepata uwekezaji mkubwa.” Amebainisha Mhe. Katimba.

Baadhi ya wananchi wa Kakonko waliojitokeza kumlaki na kumsikiliza Naibu Waziri Mkuu na waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko.

Aidha, amewahimiza wananchi wa Kakonko kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na  baadae kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kakonko na Diwani Kata ya Gwarama, Bw. Fidelis Nderego amesema “ Kakonko tukipata barabara ya kiwango cha lami hadi Soko Kuu la ujirani mwema kati ya Kakonko na Burundi uchumi wa wananchi wa Kakonko na Mkoa wa Kigoma utafunguka kiuchumi.”

Aidha, mkazi wa Kakonko, Maita Paschal amesema kuwa uwepo wa Hospitali hiyo ya Wilaya ya Kakonko unawasaidia wananchi kupata huduma karibu kuliko ilivyokuwa awali ambapo walisafiri umbali mrefu kupata huduma.

 “ Huduma sasa ni nzuri na zipo karibu na nyumbani, awali nilijifungua watoto wangu kumi hospitali ya mbali Mgaza lakini sasa tunapata huduma karibu na nimekuja kumuona mwanangu ambaye amejifungua hapa”. Amesema Maita.

Hii ni mara ya kwanza kwa Dkt. Doto Biteko kufanya ziara wilayani Kakonko tangu alipoteuliwa kuwa naibu waziri mkuu na Waziri wa Nishati.

Mwandishi: Immaculate Makilika 

Mhariri: Prosper Kwigize

Post a Comment

0 Comments