Shigela awaonya wakazi wa Geita kujichukulia Sheria mkononi.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amewaonya wakazi wa kata ya Lulembela wilayani Mbogwe Mkoani Geita kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani vitendo hivyo vimekuwa vikichangia mauaji ya watu wasio hatia katika maeneo tofauti nchini.

Amebainisha hayo Septemba 13,2024 katika ibada ya mazishi ya msichana Teresia John (18), Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya sekondari Lulembela aliyeuwawa kwa kupigwa risasi katika vurugu za Wananchi zaidi ya 800 kuvamia Kituo hicho cha Polisi Lulembela kwa nia ya kuwachukua washukuwa wa matukio ya wizi wa watoto.

"Kwa watu wanaojitambuwa halikutakiwa kutokea  hii, vaa viatu kwa yule baba aliyekuwa amebeba wale watoto harafu jamii ikugeuke uwe sehemu ya adui  hili ni  kitu ambacho hakikubaliki katika jamii"Amesema Shigela.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Lulembela Deus Lyankando amenukuliwa na kituo cha radio cha Storm FM ya Geita akimwomba  mkuu wa mkoa  Geita  kurejesha  huduma za kipolisi katika eneo hilo kwani tangu uvamizi ufanyike huduma hiyo imesitishwa katika Kata hiyo.

Taarifa iliyotolewa  September 11,2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ilisema chanzo cha tukio hilo ni baada ya Watu wawili kuonekana wakiwa wamebeba Watoto wawili na wananchi waliokuwa katika mnada wa Lulembela kuwahisi kuwa ni wezi wa watoto na kuanza kuwashambuilia, 

Waliouawa katika vurugu hizo ni Teresia John (18), mkazi wa eneo jirani na kituo hicho cha polisi ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lulembela, na mwanamume anayekadiliwa kuwa na miaka 18 hadi 20 ambaye majina yake hayajatambulika.

Maandamano ya kuvamia vituo vya polisi yamekuwa yakujirudia ambapo Agosti 21, 2024 Mji wa Lamadi wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu yalifanyika maandamano na kuvamia kituo cha Polisi.

Mwandishi; Sharifat Shinji

Post a Comment

0 Comments