Tamko kwa Wataalam wa tathimini Kuilinda Taaluma zao.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko amezitaka taasisi za ufutiliaji na tathmini kufanya kazi kwa weledi na kuimarisha eneo hilo ili kuendana na mahitaji yanayolenga kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ameyabainisha hayo leo Septemba 20, 2024 akimuwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika Kongamano la Tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza. huko Visiwani Zanzibar na kusema  wataalam wa ufuatiliaji na tathmini wanawajibika kuilinda taaluma hiyo.

"Inawezekana katika maeneo yenu ya kazi wakawepo wakuu wa taasisi au viongozi wa serikali ambao hawapendi mfanye kazi yenu vizuri, kukabaliana na hilo ni kujiua wenyewe. Mnapotoka hapa mkafanye mkuu wa taasisi au kiongozi aone umuhimu wenu katika shirika"Amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine ameielekeza Ofisi hiyo kukamilisha Sera ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ili iwezeshe utekelezaji sahihi wa eneo la ufuatiliaji na tathmini nchini. Sambamba na TanEA na ZaMEA kuweka mikakati ya kujiimarisha kiuchumi ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa uanzishwaji wake.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi amesema kuwa Kongamano hilo la tatu la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza limepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau na washiriki.

Aidha Mhe. Lukuvi amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa vinara wa ufuatiliaji na tathmini katika utendaji wa Serikali kwa ujumla.

Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa kupitia Kongamano hilo wamepata fursa mbalimbali ikiwemo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa wataalamu. Sambamba na washiriki kujifunza mbinu mpya zakuboresha mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini, hasa kwa kutumia teknolojia na takwimu sahihi ili kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.

"Kongamano hili limesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mchakato mzima wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha Serikali na wahisani wanatoa huduma zenye tija. Pia, ushirikishwaji wa waananchi utasaidia kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inawafaidisha moja kwa moja" Amesema Dkt. Yonazi.

Kongamano hilo lenye kauli mbiu isemayo "Kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia katika  ufuatiliaji na tathmini na matumizi ya matokeo ya tathmini katika kufanya maamuzi" limekuwa na mwitikio mkubwa wa washiriki ikiwa Naibu waziri mkuu na Waziri wa Nishati  Dkt. Dotto Biteko akimwakilisha Waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Mwandishi; Immaculate Makilika

Mhariri; Sharifat Shinji


Post a Comment

0 Comments