Kilio cha maji safi Mtaa wa Mkombozi chamalizika

 

Wakazi wa mtaa wa Mkombozi kata ya Murusi Halmashauri ya  mji Kasulu, mkoani   Kigoma wameishukuru Serikali pamoja na Taasisi ya Hope of the community Foundation kwa kuwaboreshea miundombinu  ya chemichemi ya maji katika mtaa wao.

 Wakizungumza na Buha News  Septemba 26,2024 baadhi ya wanufaika wa mradi huo akiwemo Ester Ibrahim, wamesema wamekuwa na  changamoto ya hupatikanaji wa maji kwa muda mrefu kutokana na chanzo  cha maji kilichokuwepo awali  kutumika kwa  shuguli zote  za  mifugo na wanadamu.

 "Miaka ya nyuma maji haya yalikuwa yanatoka machafu sana na pia tulikuwa tunachangia pamoja na mifugo, lakini pia watu walikuwa wanafua kwenye chanzo hicho , lakini kwa sasa baada ya kujengewa chemichemi tunafaidika kwa kutumia maji safi na salama ambayo yanatupa uhakika wa afya zetu kuwa salama"alisema Ester Ibrahim mnufaika wa mradi.

 Nae mkurugenzi wa Taasisi ya Hope of the Community Foundation  Bi.Eveline Leonard Kahembe amesema  taasisi hiyo ilibaini changamoto  ya maji katika eneo hilo,hivyo kuchukua hatua ya kutatua  changamoto hiyo kwalengo la kuwa epusha wakazi wa eneo hilo na magonjwa ya mlipuko ambayo husababishwa  na uchafuzi wa maji katika vyanzo vya maji.

 "Tumetembelea chemichemi 5 ndani ya wilaya ya Kasulu Mji  tukabaini uwepo wa changamoto hiyo na adha wanayo pitia wakazi wa maeneo haya tukaona ni vyema sisi kama taasisi kurudisha faida kwa wananchi kwa kuwaboreshea miundombinu ya chemichemi hizo"alisema Eveline.


               Chanzo cha maji kilichoboreshwa katika kata ya Mkombozi 

Nae Afisa mazingira wilaya ya Kasulu mji Bw.Msafiri Charles ameshukuru   uboreshaji wa chemichemi hiyo, na kuwaomba wadau zaidi kujitokeza kuungana na jitihada za serikali katika kuhakikisha wakazi wa mji wa Kasulu wanapata maji safi na salama.

Aidha Bw. Msafiri amesema serikali na wadau wamekuwa wakipeleka miradi ya maendeleo katika jamii   hivyo amewaomba wananchi  kuhakikisha wanatunza miradi hiyo ikiwemo chanzo hicho cha maji ili waendelee kupata maji safi na salama.

Mpaka sasa Halmashauri ya mji Kasulu kwa kushirikiana na wadau  wa maendeleo na  mazingira wameboresha  chemichemi tano katika maeneo tofauti  ikiwemo Mudyanda, Sunzu, Kanazi, Murusi na Msambala .

Mwandishi: Ellukaga Kyusa 

Mhariri:Harieth Dominick 

Post a Comment

0 Comments