Zanzibar yatembelea vyuo vya FDC's

 

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetembelea vyuo vya Maendeleo ya Wananchi nchini (FDC's) kwa lengo la kujifunza namna vyuo hivyo vinavyotoa mafunzo na ujuzi kwa vijana hususani kwa wanawake vijana waliokatiza masomo kutokana sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na hali ngumu ya maisha.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC, Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanahamisi Ameir amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi kutoka katika vyuo hivyo na kuboresha vituo vya mafunzo mbadala Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanahamisi Ameir akitoa maelekezo kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi FDC's jijini Dar es Salaam. (picha: michuzi)

Aidha ameongezea kuwa  Zanzibar kupitia Mamlaka ya Mafunzo ya Amali wanatoa elimu mbadala katika vituo vya Raha Leo na Pemba katika kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi na kupitia ziara hiyo watachukua baadhi ya mambo ili kuboresha zaidi vituo vya elimu mbadala na kuwaalika wakufunzi na wadau wa FDC's  kutembelea vituo hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa KTO Maggid Mjengwa amesema, ujio wa ugeni huo utaleta hamasa na chachu ya uelewa wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania na kufikia 2025 Falsafa ya muasisi wa vyuo hivyo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoianzisha mwaka 1975 hivyo vitatimiza miaka 50 kwa mafanikio makubwa.

Pia Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni FDC Eng. Ramadhan Simba amesema ujio wa viongozi hao umewapa ari zaidi ya kuwahudumia vijana hao pamoja kuongeza ubunifu zaidi kwa manufaa ya Taifa.

Katika hatua nyingine amewataka wananchi hususani vijana kutokata tamaa na kutumia kutumiafursa hizo zinazotolewa katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 nchini kupata elimu na ujuzi na hatimaye kuendelea na ngazi nyingine za Elimu.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya KTO Shaban Lugome amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa hususani katika utoaji wa elimu kwa vijana na KTO wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi utakaoleta tija kwa jamii kwa kupunguza changamoto ya ajira.

Mwandishi; Abel Mahenge

Post a Comment

0 Comments