Zitto Kabwe abisha hodi Bungeni uchaguzi ujao

Kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Zuberi Kabwe amesema hana mpango wa kugombea Urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2025 huku akitaja kuwania nafasi ya Ubunge jimboni kwake.

Bw. Kabwe ambaye kustaafu kwake kuwa kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo kuliacha maswali mengi amebainisha hayo leo Septemba 04 wakati akifanyiwa mahojiano na Crown media ya Jijini Dar es Salaam.

Kabwe ambaye ni miongoni mwa wanasiasa machachali amebainisha kuwa uchaguzi uliopita ulizalisha wabunge wa chama kimoja hivyo kwa mwaka huu wamejipanga kwenda na jopo la idadi kubwa ya wabunge kutoka katika chama  hicho.

Amesisitiza kuwa kurejea kwake bungeni kutasaidia kurejesha siasa ya ushindani nchini hata Bungeni huku akibainisha kwamba mchakato wa kuwapata wagombea watakaopigiwa kura kwa ngazi za serikali za mitaa unaendelea.

Zito Zuberi Kabwe amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na baadaye jimbo la Kigoma mjini kabla ya kushindwa katika uchaguzii wa mwaka 2020 ambapo Kirumbe Ngenda kutoka Chama Cha Mapinduzi alishinda na kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Mwandishi: Abel Mahenge 

Post a Comment

0 Comments