Bilioni 3 kutatua changamoto ya Barbara Lindi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepeleka fedha za ujenzi wa barabara mkoani Lindi na amemwagiza Meneja wa TANROADS wa mkoa huo, Mhandisi Emil Silas Zengo ahakikishe barabara ya Kata ya Milola inawekwa lami mapema iwezekanavyo.

Amefikia hatua hiyo baada ya Mhandisi Zengo kukiri kuwa walishapokea fedha kiasi cha sh.bilioni 3.5 ambazo  zililenga kujenga barabara ya Milalo Centre yenye urefu wa kilometa nne, kujenga mitaro na kuweka taa za barabarani. 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo jioni (Ijumaa, Oktoba 18, 2024) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kijiji cha Milola, kwenye mkutano uliofanyika kwenye senta ya Milola,  kata ya Milola, wilayani Lindi.

Mhandisi huyo amesema Jumatatu ijayo (Oktoba21, 2024), wataalam wataenda kwenye kata hiyo ili waweze kuanza kazi ya usanifu na hatua nyingine za msingi zitaendelea ili baada ya mwezi mmoja, mkandarasi aanze kazi.

Wakati huohuo,  Waziri Mkuu amesema Serikali ya Rais Samia imekwishatoa sh. bilioni 1.8 kwa ajili ya miradi mbalimbali kwenye sekta za elimu na maji.

Waziri Mkuu amesema pia atafuatilia ahadi za Serikali kuhusu ujenzi wa vituo vya afya vya Milola na Rutamba ili kazi hiyo ianze mara moja kwani maeneo hayo yana idadi kubwa ya watu.

Alikuwa akitoa ufafanuzi wa hoja iliyotolewa na Mbunge wa jimbo la Mchinga, Salma Kikwete ambaye aliomba ahadi ya Serikali ya ujenzi wa vituo hivyo ifuatiliwe ili kuwanusuru wananchi hao na adha ya kukosa huduma bora za afya kwani hivi sasa wanatibiwa kwenye zahanati. 

Post a Comment

0 Comments