Buha FM Radio yakabidhiwa leseni rasmi na TCRA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekikabidhi leseni kituo cha habari na mawasiliano cha Buha FM Radio kinachomilikiwa na asasi ya uwekezaji katika Utu na maendeleo OHIDE kinachorusha matangazo yake kutoka Mjini Kasulu mkoani Kigoma.

Hafla hiyo imefanyika mapema leo jijini Dodoma ambapo Meneja wa mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati  Dodoma Mhandisi Asajile Mwakisisile amemkabidhi leseni hiyo Mkurugenzi na mwasisi wa Buha Media Bw. Prosper Kwigize

Akikabidhi cheti hicho mhandisi Asajile amepongeza asasi ya OHIDE kwa kuona umhimu wa kuwekeza katika sekta ya mawasiliano na habari katika maendeleo ya mikoa ya pembezoni na kuihimiza uzingatiaji wa maudhui yanayoleta tija kwa umma

"Nakupongeza sana kwa kuona umhimu wa kuongeza huduma za upashanaji wa habari mkoani Kigoma, tuna imani kuwa kituo cha Buha FM Radio na mtazingatia maadili na kanuni za utangazaji" amesisitiza meneja wa TCRA Kanda ya Kati Mhandisi Asajile

Kwa upande wake Mkurugenzi na mwasisi wa OHIDE na Buha Radio na Runinga mtandaoni ya Buha Bw. Prosper Kwgize ameshukuru serikali na mamlaka ya mawasiliano kwa kukubali maombi ya kuanzisha kituo hicho.

Kwigize pamoja na shukurani hizo ameahidi kushirikiana na serikali na wadau wengine wa maendeleo kuzalisha maudhui yatakayoleta matokeo chanya kwa jamii ikiwa ni pamoja na ukuaji wa uchumi na mahusiano ya kimataifa.

Mtangazaji dada Shukuru Imana akitekeleza wajibu wake katika studio za Buha FM mjini Kasulu

Kituo cha Buha FM Radio kinarusha matangazo yake kupitia masafa ya 100.1 kutokea Mwilamvya mjini Kasulu mkoani Kigoma na kinasikika karibu mkoa mzima wa Kigoma na maeneo yake ya jirani sambamba na kambi za wakimbizi kutoka Burundi na jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Miongoni mwa vipindi vinavyopewa kipaumbele ni pamoja na mazingira, Uchumi na biashara, utetezi wa haki za watoto, wanawake na wazee, uhamiaji na wakimbizi, na mahusiano ya kimataifa baina ya nchi za jumuiya ya Afrika mashariki.

Aidha matangazo ya Buha FM yanasikika kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo tovuti ya www.buhanews.co.tz na kupitia mitandao ya kimataifa ya Radio Box, My tuner, Zeno Radio na Radio Garden ambapo inazifikia nchi zote duniani, na habari zote zinapatikana kupitia facebook, instagram na tiktok.

Mwandishi: Mussa Mkilanya

Mhariri: Eunice Jacob

Post a Comment

0 Comments