Daktari wa viungo mbaroni kwa tuhuma za kubaka mtoto



Daktari wa viungo Haruna Ayubu maalufu kama Rubai (63) mkazi wa kata ya Rwamishenyi manispaa ya  Bukoba amepandishwa kizimbani kwa shitaka la ubakaji wa mtoto wa miaka 12.

Rubai amefikishwa katika mahakama ya wilaya Bukoba Oktoba 23 mwaka huu na kusomewa kesi ya jinai namba 30251/2024.

Upande wa mashtaka unaongozwa na mawakili wawili ambao ni Matilda Assey pamoja na Alice Mutungi.

Akisoma maelezo ya awali wakili upande wa mashtaka Matilda Assey amesema kuwa, kati ya Desemba 2023 na Oktoba 19, mwaka huu  mshitakiwa amekuwa akimuingilia mhanga katika moja ya chumba katika ofisi yake iliyopo mtaa wa Pwani, kata ya Miembeni manispaa ya Bukoba.

Assey alieleza mahakama kuwa, mshitakiwa amekuwa akimwingilia mtoto huyo (jina linahifadhiwa) na kisha kumpatia sh. 10,000 au 5,000 kwa ajili ya kuwapelekea wazazi wake.

Aidha alisema, Oktoba 19, mwaka huu mhanga alikwenda tena katika ofisi ya mshitakiwa kwa lengo la kuchukua fedha ambayo amekuwa akimpatia kama msaada na baada ya mhanga kufika mshitakiwa alimpeleka katika chumba kisha kumbaka na baada ya hapo alimpatia sh.1,000 akanunue soda.

Mhanga alipelekwa hospitali na daktari alithibitisha kuwa ni kweli aliingiliwa kutokana na michubuko sehemu ya uke wake akimaanisha kuwa mhanga alikuwa ameingiliwa.

Upelelezi wa shauri hilo umekamilika wapo tayari kuendelea na kesi na upande wa mashtaka wana mashahidi 10, vielelezo vya maandishi vitatu na ripoti ya daktari.

Wakili wa upande wa utetezi  Frank  John, aliieleza mahakama hiyo kuwa hawako tayari  kuendelea na kesi  jana ( leo ) na kudai kuwa ili mshtakiwa aweze kusikilizwa kikamilifu lazima awe amepewa maelezo ya mlalamikaji.

Wakili John, alisema pamoja na kusomewa shitaka bado mshitakiwa hajapewa hati ya mashtaka na hoja ya tatu  apate muda wa kuongea na mteja wake ili aone ni jinsi gani ya kuweza kumtetea vizuri katika shtaka linalomkabili na ndiyo msingi muhimu wa haki ya kuwakilishwa na wakili.

Pia aliiomba mahakama kuahairisha shauri hilo kwa tarehe nyingine  ambayo watakubaliana bande zote mbili upande wa utetezi na upande wa mashtaka kwa sababu siku moja kabla ya kesi hiyo alipata msiba wa kufiwa na kaka yake.

Akijibu hoja za wakili wa upande wa utetezi wakili wa Serikali  Alice Mutungi alisema mshitakiwa alifikishwa mahakamani tangu asubuhi hadi saa kumi jioni kama alitaka kuongea na mteja wake wangekuwa wameshaongea na kuiomba mahakama kuangalia maslahi  ya mtoto ambaye ni mhanga katika shauri hilo ambaye pia amekuwepo mahakamani hapo tangu asubuhi kwa ajili ya kusikilizwa.

"Tukisema shauri hili lihairishwe mtoto aondoke na kurudi tena tunaona kwa mazingira haya sio salama kwa mtoto, tunaiomba mahakama yako tukufu kwa maslahi ya mtoto shauri hili lisikilizwe kwa haraka ili mtoto asiwe anakuja mahakamani na kurudi"alisema wakili Alice.

Alisema  hati ya mashtaka alipewa wakili wa mshitakiwa na wakili hajakana amekiri kupokea hati hiyo kisheria wakili ni muwakilishi wa mshitakiwa na yupo kwa ajili ya kumsemea.

Hakimu wa mahakama ya wilaya Endrew Kahabuka baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, upande wa wakili wa utetezi na upande wa mawakili wa mashitaka aliwataka upande wa utetezi kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni wadhamini wawili wakazi wa manispaa ya Bukoba wenye mali zisizohamishika zenye thamani ya sh. milioni nne kila mmoja na mtuhumiwa kutakiwa kutotoka ndani ya manispaa ya Bukoba labda kwa kibali maalum cha mahakama.

Upande wa utetezi walitimiza masharti hayo na mshitakiwa akapata dhamana,  hata hivyo, alikamatwa tena akiwa amefika nyumbani kwake.

Kesi hiyo ilihahirishwa na itatajwa tena Oktobaa 19,mwaka huu.

Mwandishi: Ananias Khalula, Bukoba

Mhariri: Prosper Kwigize

Post a Comment

0 Comments