Fursa ya Umeme vijijini iwe chachu ya matumizi ya Nishati safi -Mhe.MHAGAMA

 

Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama amesema juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Nishati kufikisha umeme hadi maeneo ya Vijijini zinapelekea wananchi kupika kwa kutumia nishati iliyo safi kupitia majiko yanayotumia umeme kidogo.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo Octoba 4,2024 jijini Dodoma  wakati akihamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi na kuanza kupika kisasa kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia.

"Kutokana na uwepo wa umeme katika Vijiji, sasa Mwanamke mahali popote Tanzania anaweza kupika kisasa kwa kutumia nishati safi badala ya kuni na mkaa ambazo si nishati safi." Amesema Mhagama.

Amesema faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia zinakwenda hadi katika ngazi ya familia kwa namna mbalimbali ikiwemo kuimarisha afya za wana familia.

"Magonjwa yanapoondoka kwenye familia hata gharama za matibabu zinaondoka na kama hakuna gharama za matibabu ina maana nguvu inaelekezwa katika maendeleo ya familia." Ameeleza Mhagama.

Ametoa rai kwa jamii kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi kutokana na uharibifu wa mazingira kupitia ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa  hivyo kusababisha madhara mbalimbali  ikiwemo mafuriko na mvua zisizotabirika.

kampeni ya Serikali ni kuhakikisha inaendelea kutoa  hamasa kwa jamii ili  asilimia 80 ya Watanzania watumie  nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.

Na mwandishi Wetu .

Post a Comment

0 Comments