Maagizo ya Dkt. Biteko kuzingatiwa ujenzi wa ofisi ya Wizara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba leo ameongoza Menejimenti ya Wizara ya Nishati kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara hiyo katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma. 

Akiwa katika jengo hilo alielezwa na Msimamizi wa ujenzi wa jengo kutoka Wizara ya Nishati, Alphonce Kilovele kuwa, ujenzi umefikia asilimia 84.3 na kwamba ifikapo mwezi Januari 2025 litakuwa tayari kwa matumizi.

Kilovele ameieleza Menejimenti ya Wizara ya Nishati kuwa, kazi zinazoendelea sasa ni za umaliziaji wa huduma saidizi ikiwemo miundombinu ya umeme, maji, zimamoto, Tehama, viyoyozi na vioo. 

Ameeleza kuwa, jengo hilo litakalochukua watumishi 200 hadi 300 linafungwa mifumo ya umeme inayozingatia matumizi bora ya Nishati (energy efficiency) ikizingatiwa kuwa Wizara ya Nishati ni kinara wa usimamizi wa matumizi bora ya nishati nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (wa nne kushoto) pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakimsikiliza Msimamizi wa ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati, Alphonce Kilovele (wa kwanza kushoto)  wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Mramba amewakumbusha wasimamizi wa jengo hilo kuhakikisha kuwa agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko la majengo yote ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kufungwa mifumo ya nishati jadidifu ikiwemo umeme Jua linazingatiwa.


 

 

Post a Comment

0 Comments