Macron atoa tamko zito juu Ya Sahara magharibi na Morocco


Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameliambia bunge la Morocco kwamba anaamini Sahara Magharibi inapaswa kuwa chini ya mamlaka ya Morocco, na ameahidi kuwekeza fedha za Ufaransa huko.

Sahara Magharibi ni eneo la pwani ya kaskazini-magharibi mwa Afrika ambalo limekuwa na mzozo kwa miongo kadhaa.

Wakati fulani lilikuwa koloni la Uhispania, na sasa linadhibitiwa zaidi na Morocco na kwa kiasi fulani na Polisario Front inayoungwa mkono na Algeria, ambayo inasema inawakilisha watu asilia wa Sahrawi na inataka taifa huru.

Ufaransa ilikuwa nchi yenye nguvu ya kikoloni katika nchi ya Morocco na Algeria. Inaungana na mataifa mengine ikiwemo Uhispania, Marekani na Israel kuunga mkono mpango wa Morocco.

Wabunge walisimama na kumpongeza Macron Jumanne aliposema, "kwa Ufaransa, eneo hili la sasa na la siku zijazo liko chini ya mamlaka ya Morocco".

 Akiashiria mabadiliko katika msimamo wa muda mrefu wa Ufaransa kuhusu mpango wa Morocco wa kuipa Sahara Magharibi uhuru wa kujitawala chini ya mamlaka ya Morocco, rais wa Ufaransa alisema huo ndio "msingi pekee" wa suluhu ya haki na ya kudumu ya kisiasa.

Uungaji mkono wa Ufaransa kwa madai ya eneo la Morocco uliikasirisha Algeria, ambayo ilijibu habari hiyo kwa kumuondoa balozi wake huko Paris.
 Algiers inachukulia uwepo wa Morocco huko kama uvamizi haramu.

Wachambuzi wanasema uamuzi wa Ufaransa kuunga mkono madai ya Morocco ni jaribio la kurekebisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, ambao ulikuwa umedorora baada ya Rabat kushutumiwa kwa kujaribu kufanya ujasusi dhidi ya Rais Macron na Ufaransa ikaimarisha vikwazo vya visa kwa raia wa Morocco wanaozuru nchni humo.

Uhusiano kati ya Morocco na Algeria umekuwa wa wasiwasi hasa katika miaka ya hivi karibuni, na Algiers ilitangaza mwaka 2021 kwamba ilikuwa imekata uhusiano wa kidiplomasia na jirani yake wa magharibi.

Mwandishi :Eunic Jacob
Mhariri : Ellukagha Kyusa 




Post a Comment

0 Comments