Nchi ya Mali yavutiwa na mafanikio sekta ya Mawasiliano , TEHAMA Tanzania


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amepokea na kuikaribisha timu ya wataalamu kutoka nchi ya Mali kwa ajili ya kujifunza kutoka katika Serikali ya Tanzania namna kuratibu na kusimamia masuala yote yanayogusa tasnia ya mawasiliano na TEHAMA.

Akizungumza na ujumbe huo leo  Oktoba 24, 2024 Jijini Dodoma, Bw. Abdulla amesema Wizara hiyo na taasisi zake wapo tayari kutoa ushirikiano kwa kuwa kuna maeneo mengi ambayo nchi ya Mali inaweza kujifunza Tanzania yakiwemo masuala ya akili mnemba (AI).

 “Kama nchi kupitia Wizara hii tuna mafanikio na mipango mingi ambayo ipo kwenye hatua za utekelezaji ikiwa ni pamoja na kujenga chuo kikubwa cha umahiri cha TEHAMA na Kituo kikubwa zaidi cha kuhifadhia Data hivyo mnakaribishwa sana kujifunza kutoka kwetu”, amesisitiza Abdulla

 Naye Bw. Ibrahima Abdoulaye Kone, kiongozi wa wataalamu hao wa Mali amesema kuwa Mali ina mengi ya kujifunza kutoka Tanzania hasa katika muundo wa kitaasisi, umoja na ushirikiano uliopo kwa taasisi zinazoshughulikia masuala ya mawasiliano na TEHAMA.

Kone Amesema kuwa, nchini Mali, uratibu na usimamizi wa taasisi zinazojihusisha na masuala ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA haupo katika Wizara moja kama ilivyo kwa Tanzania hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kushindwa kuratibiwa vema.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla akipokea zawadi kutoka kwa Bw. Ibrahima Abdoulaye Kone, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Masoko wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano na Posta ya Mali (AMRTP) akiongoza  timu ya wataalamu kutoka Mali waliofika Wizarani hapo leo Oktoba 24, 2024 jijini Dodoma kwa ajili ya kujifunza kuhusu uratibu na usimamizi wa tasnia ya Mawasiliano na TEHAMA.

Ameongeza kuwa asilimia 99 ya wananchi wa Mali wanamiliki simu janja ambapo bei ya kifurushi cha data kwa GB moja ni sawa na dola za kimarekani mbili sawa na shilingi 5500 fedha za kitanzania.

Wataalamu hao kutoka Mali wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano na Posta ya Mali (AMRTP) na Wakala wa Usimamizi wa Mfuko wa Upatikanaji wa Huduma za Mawasiliano kwa Wote (AGEFAU) waapo nchini kuanzia Oktoba 21 hadi 26, 2024 kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na Wizara Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF); Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); na kampuni ya simu ya Airtel.

Na mwandishi Wetu.

Post a Comment

0 Comments