Pamoja na Matokeo chanya ya Elimu ya kilimo soko bado Kitendawili kwa wakulima Kasulu Mji

 Kufuatia agizo la Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano  Tanzania Kasimu Majali alilotoa wakati  akiahirisha shughuli za Bunge la 12 mkutano wa 16 jijini Dodoma aliagiza Maofisa ugani wote kuwatembelea wakulima na kuwapa elimu ya kilimo  inayoendana na Mabadiliko ya hali ya hewa  ili kulinda usalama wa chakula Nchini .

Buha News imemtafuta Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya mji wa Kasulu  Zephania Sodya   kufahamu ikiwa tayari utekelezaji wa agizo hilo  umeanza mjni hapa .

Akizungumza na Buha News, Bw.  Zephania Sodya  amesema kwa kushirikiana  na shirika la World Vision kupitia Mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) wenye lengo la kuhamasisha kilimo cha mazao ya Mahindi,Alizeti na Maharage  wameendelea kutoa elimu kwa wakulima kuanzia upandaji wa Mbegu hadi kuvuna mazao kwa  kata zote.

“Tunawafikishia wakulima elimu hiyo hata kabla ya agizo la waziri mkuu  ,elimu ya  namna ya kupata mbolea ya ruzuku,aina ya mbegu za kupanda kulingana na eneo husika  na  tunafuatilia maelekezo ya mamlaka ya hali ya hewa ili tuweze kuwasaidia wakulima na hatuna shaka wakulima wanaelimu ya kutosha kwasababu tuna wakulima viongozi wanaoongoza vikundi vya wakulima katika kata zote” anasema Bw. Sodya.

Afisa kilimo pia amesema upatikanaji wa mbolea ya ruzuku ni toshelevu kwa mji wa Kasulu hivyo amewashauri wakulima wasiyo na namba kujisajili mapema ili wapate Namba itakayowawezesha kupata mbolea ya Ruzuku  na  kusisitiza wakulima waliosajiliwa mwaka jana watatumia namba zao za awali .

Wakizungumza na Buha News ,kwa njia simu wakulima kutoka kata tofauti  akiwemo Dorothea Ntibinona kutoka kata ya Mhunga kijiji cha Marumba amekiri kupata elimu ya  kilimo chenye tija na kwamba elimu inaendelea kutolewa kuhusiana na matumizi ya mbegu bora , ,mbolea na viwatiliu ingawa changamoto kubwa walionayo ni ukosefu wa masoko ya mazao yao.


Mafunzo ya kilimo  tija yanayosimamiwa na Halmashauri ya mji wa Kasulu  kwa kushirikiana na World  Vision  yakiendelea katika kata ya Msambara .

Bi Dorothea ameongeza kuwa  changamoto nyingine ni ukosefu wa pembejeo za Ruzuku katika maeneo yao ,hivyo hulazimika  kusafiri kwa gharama za ziada kufuata Pembejeo mjini hali inayoongeza  usumbufu na kupoteza muda wa kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo .

“Nauli ya kutoka hapa kijijini ni 4000 kwenda na kurudi 8000 bado ujalipa ghrama ya kubeba  Mbolea kutoka Kusulu hiyo gharama kubwa kwa mkulima  kumbuka mazao tunapata, ila  hatuna soko la kuuza kwahiyo hizo ndiyo changamoto zetu “Alisema Dorothea .

Nae  mkulima kutoka kata ya  Nyachenda ambaye hakupenda jina lake litajwe amekiri kufikiwa na elimu ya kilimo bora ambayo imeleta mbadiliko chanya  kwa wakulima,na  uzalishaji  wa mazao umeongezeka lakini anataja changamoto ya soko kuwa kizungumkuti hali inayoendelea kusababisha umaskini kwa wakulima.

 “Mwanzo nilikuwa nalima robo heka napata debe nne  au tatu pekee lakini baada ya kupata elimu ya kilimo bora ,nikaanza kulima zao moja mwanzo tulikuwa tunachanganya mazoa ,nikaanza kufua na sentimita za kupishana kati ya mbegu moja na nyingine nazingatia pia aina za mbegu kulingana na hali ilivyo ,nafuata pia utaratibu wa uwekaji mbolea na kwasasa  navuna hadi gunia  4 hadi 5 kwa robo heka, lakini hakuna soko la kuuzia” Alisema mkulima huyo.

Kwa upande wake  Kiongozi wa wakulima kutoka kijiji cha Marumba Kata Muhunga anayeongoza vikundi zaidi ya sita vya wakulima  katika eneo hilo  Asela Richard Lulangara amesema elimu imewafiki  na wameongeza uzalisha lakini bado kuna changamoto ya ukosefu wa soko pamoja na upatikanji wa mbolea katika maeneo yao ,ambapo  wameitatua chanamoto hiyo ya kukosa mbolea  kwa kushirikiana na shirika la World Vision Kigoma  kupitia Mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI)  wanawasaidia  wakulima kupata mdau anayeleta mbolea katika maeneo yao.

“Tunakusanya Hela zetu kupitia kuweka hisa kisha kila mkulima ananunua mbolea kulingana na uhitaji wake alafu World Vision wanatutafutia mdau anayeleta mbolea kijijini kulinga na mahtaji ya wakulima ” alisema Bi.Asela .

                                            Picha kutoka maktaba 

Katika hatua nyingine  Bi. Amina Yusuph mkulima kutoka Kata Kidyama amesema yeye hajabahatika kupata elimu ya Kilimo bora na anaendelea kulima kilimo cha za zamani .

“Mimi sijawai kuwaona maafisa  kilimo labda wakipita huku  huwa nakuwa nyumbani au kwenye biashara zangu nyingine” alisema Bi Amina.

Akizungumzia changamoto ya ukosefu wa Soko la mazao Ofisa Kilimo Halmashauri ya mji Kasulu Bw. Zephania Sodya  amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo kwa wakulima na kubainisha kuwa wanaendelea kukabiliana na changamoto hiyo kwa kushirikiana na maofisa ushirika  kuanzisha vyama vya Ushirika ambavyo vitasaidia upatikanaji wa soko kwa wakulima.

“Tayari tumeanzisha AMCOSS kata ya Mwilamvya,Kijiji cha Ruhita,kijiji cha Karuta ,Mwanuhe kata ya Heru juu na Kata Msambara Lengo ni kuwawezesha wakulima kupata masoko ya kuuza mazo yao kupitia vyama vyao vya ushirika na tunatarajia ndani ya miaka 3 ijayo wakulima wataanza kuona matokeo chanya ya vyama hivi ” Alisema Afisa Kilimo.

Kuhusu upatikanaji wa Mbolea ya Ruzuku Ofisa kilimo huyo amesema wako baadhi ya mawakala wanaopeleka mbolea vijijini lengo ikiwa nikuwasaidia wananchi wapate mbolea hizo maeneo yao.

Mamlaka ya hali ya hewa  Tanzania (TMA) ilitoa utabiri  wa hali ya hewa  Mwezi Agusti mwaka huu ,wakati wakitoa mwelekeo wa mvua kuanzia Mwezi Octoba  hadi Desemba 2024 ulionesha uwepo wa upungufu wa mvua za msimu wa vuli,utabiri uliomfanya waziri mkuu wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Kasimu Majaliwa  kutoa maelekezo kwa maafisa ugani nchi nzima  ili kuepuka upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza kwa kutokuchua tahadhari ya mapema .

Mwandishi:Harieth Kamugisha 

Mhariri: Sharifat Shinji

Post a Comment

0 Comments