Rais Dkt. Samia akamilisha mbio za Mwenge wa Uhuru

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa maono na fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zinaendelea kuishi, na Taifa la Tanzania linaendelea kujivunia amani, mshikamano na umoja.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa historia ya Mwalimu Nyerere haiwezi kutofautishwa na historia ya Mwenge wa Uhuru, ambayo ni Tunu ya Taifa ambayo Mwalimu Nyerere amewaachia Watanzania.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo wakati wa Kumbukizi ya Miaka 25 ya Kifo cha Hayati Mwalimu Nyerere na Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Rais Dkt. Samia amewapongeza vijana walioshiriki mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2024 kwa kuzunguka nchi nzima kuhamasisha shughuli za maendeleo na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii, kuwajibika na kuwa wazalendo kwa Taifa lao.

Wakimbiza Mwenge kitaifa katika gwaride la utabulisho kabla ya kukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza 

Vilevile, ameeleza kuwa Serikali itafanyia kazi taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Ndugu Godfrey Eliakim Mzava inayojumuisha changamoto, maombi na ushauri uliotolewa na wananchi kupokelewa na Mwenge wakati wa mbio hizo.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa vijana kuendelea kulinda Mwenge wa Uhuru ambayo ni Tunu ya Taifa na kuuenzi kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Akizungumzia Maonesho ya Wiki ya Vijana, Rais Dkt Samia ametoa pongezi kwa vijana kwa ubunifu, ujuzi, uthubutu na utayari wao walioonesha kupitia kazi zao na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili.

Mh. Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali walioshiriki kilele cha wiki ya vijana na mbio za Mwenge wa Uhuru 

Katika kuchochea zaidi ubunifu wa vijana, Rais Dkt. Samia ameelekeza Halmashauri zote nchini kununua vifaa vinavyotumika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kufundishia wanafunzi ambavyo vinazalishwa kwa ubora na vijana wabunifu hapahapa nchini.

Rais Dkt. Samia pia amerejea wito wake kwa wananchi kujiandikisha ili waweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ikiwa ni kuendana na dhamira ya Uhuru ya kuwawezesha wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe, ikiwemo kwa kuwachagua viongozi wao.


Post a Comment

0 Comments