Rais Samia ajiandikisha kuwa mpiga kura Chamwino

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kutimiza haki yao kikatiba ya kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo wanapoishi.

Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo mara baada ya kushiriki katika zoezi rasmi la uandikishwaji kwenye daftari hilo lililofanyika katika ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Chamwino Ikulu, Kitongoji cha Sokoine.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika kituo hicho, Rais Dkt. Samia amewapongeza kwa kujitokeza kwa wingi, pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kushiriki zoezi hilo la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na utulivu.

Uandikishwaji katika Daftari la Mpiga Kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeanza rasmi leo na utaendelea hadi tarehe 20 Oktoba, 2024.

Aidha, kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (Public Holidays Act) Sura 35, Rais Dkt. Samia ametangaza tarehe 27 Novemba, 2024 kuwa siku ya mapumziko ili kuwaruhusu wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mwandishi: Sharifa B. Nyanga

Mhariri: Prosper Kwigize


Post a Comment

0 Comments