REA yasasambaza umeme vijiji 785 Mkoani Mtwara

 

Baada ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 785 Mkoani Mtwara, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 16.7 wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150 utakaonufaisha kaya 4,950 mkoani humo.

Msimamizi wa Miradi ya Umeme REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Deogratius Nagu amebainisha hayo Oktoba, 02, 2024 Wilayani Masasi Mkoani Mtwara mbele ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Kanali Patrick Sawala wakati wa kumtambulisha Mkandarasi atakayetekeleza mradi huo Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd ya Arusha.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kukamilisha utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 785 mkoani hapa kwa asilimia 100 na sasa ni zamu ya vitongoji ambapo kiasi cha shilingi 16,717,407,821.65 kitatumika kutekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 150,” alisema Mhandisi Nagu.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa mkandarasi huyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala alizipongeza REA na TANESCO kwa kuendelea kushirikiana kuhakikisha dhamira ya Rais  ya kuwaletea wananchi  maendeleo kupitia Nishati inatimia.

“Wana Mtwara tuna kila sababu ya kuimshukuru serikali yetu  kwani kwa sasa hapa kila Kijiji kina umeme na sasa wanahakikisha umeme unafika vitongojini,” alisema Mkuu wa mkoa wa Mtwara .


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala (kulia) akipokea nakala ya mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vitongoji 150  kutoka kwa Samwel Lema  Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd ya Arusha iliyoshinda zabuni ya kusambaza umeme katika vitongoji 150 Mkoani humo.

Awali Akizungumzia utekelezaji wa mradi  huo Mhandisi Nagu ,  alisema kati ya vitongoji 3,427 vilivyopo Mkoani humo, vitongoji 2,200 vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 64 na kwamba vitongoji 150 ambavyo vitapata umeme kupitia mradi huo vitaongeza idadi ya vitongoji vyenye umeme katika Mkoa wa Mtwara.

Aidha,  ameongeza kuwa, mradi utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na  kukamilika ifikapo Septemba 2026 na kwamba utekelezaji utakuwa katika Majimbo 10 katika wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala, Masasi na Nanyumbu na kila Jimbo litakuwa na  Vitongoji 15 vitanufaika.

Kwa upande wake Mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering Works Ltd, Samwel Lema amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi utatekelezwa kwa ubora unaotakiwa na utakamilika ndani ya muda kama ilivyo katika mkataba.

Tukio hilo lilishuhudiwa na viongozi wa Mkoa na Wilaya wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Nanyumbu, Mtwara na Tandahimba, Kamati za Usalama Mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Masasi, Madiwani kutoka Kata mbalimbali Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. 


Mwandishi:Mohamed Saif

Mhariri: Harieth Kamugisha 

 

Post a Comment

0 Comments