Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo katika mkutano wa 11 wa taasisi ya Merk Foundation, uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwajumuisha wake wa marais 15 kutoka nchi za Afrika. Rais Samia aliwaomba wake wa marais, kutumia utashi, upole na kushawishi wenza wao, ambao ni marais wa sasa, kuhimiza ajenda ya matumizi ya nishati safi Afrika.
Pamoja na hilo la nishati, kadhalika Rais Samia alitumia jukwaa hilo kueleza namna serikali ya Tanzania inavyoweka kipaumbele katika elimu ya mtoto kike huku akitoa mfano wake yeye mwenyewe, na jinsi elimu ilivyomkomboa hadi kushika nafasi ya juu ya uongozi. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Merk Foundation, Afrika na bara la Asia, Dk Rasha Kelej, amesema taasisi hiyo imejikita katika kuimarisha afya, elimu kwa makundi maalum na kuondoa ukatili wa kijinsia kwa watoto barani Afrika na Asia.
Mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini hapa, uliwakutanisha wenza wa Marais kutoka nchi 15 za Botswana; Burundi; Cape Verde; Jamhuri ya Afrika ya Kati; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC); Gambia; Ghana, Liberia; Malawi; São Tomé; Zambia, Zimbabwe huku mwenyeji Tanzania ikiwakilishwa na mwenza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi.
Mke wa Rais wa Kenya, Rachel Ruto, alizungumzia nafasi na wajibu wa wenza wa marais katika mkutano huu. Mke wa Rais wa Maldives, Sajidha Mohamed, amesema jukwaa hilo linawakilisha jitihada za pamoja za kupambana na changamoto zinazokabili mataifa ya afrika. Mkutano huo wa 11 wa Merk Foundation, umewakutanisha washiriki 400 kutoka nchi 70 za Afrika huku wenza wa marais wakipewa dhamana ya kutekeleza mikakati afya, elimu, maji safi na ajenda ya nishati safi katika nchi zao.
Mwandishi :Abel mahenge
Mhariri; Ellukaga kyusa
0 Comments