Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Singapore Kibiashara utadumisha uhusiano uliopokati yake ambao umedumu kwa muda mrefu.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Oktoba 21, 2024 akiwa nchini Singapore mara baada ya kukutana na kufanya mazungunzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim Yong.
“ Tunatakiwa kujifunza kutokana na uhusiano huu na hasa kutoka Singapore kwa kuwa mmepiga hatua katika sekta ya nishati hadi kuwa na uwezo wa kufikia mahitaji ya juu ya umeme ya zaidi ya Gigawati 8, hicho ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na Tanzania yenye takribani Megawati 3000 ambapo hadi mwaka 2030 tumepanga kufikia Megawati 10,000,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha Dkt. Biteko ameipongeza Singapore kwa uzalishaji wa umeme wa jua na kusema kuwa Tanzania inaendelea na jitihada zake za kuzalisha umeme huo.
“ Mpango huo hauwezi kutokea bila kuwa na ushirikiano na wadau na nchi zingine kama Singapore, ni matumaini yetu kuona ushirikiano huu unaendelea kukua kati ya nchi zetu na kuleta manufaa kwa wananchi' alisema .
Akakizungumzia miradi ya nishati inayoendelea kutekelezwa, Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa nchi inaendelea na utekelezaji wa mradi Julius Nyerere (JNHPP)utakaozalisha megawati 2115,huku upembuzi yakinifu unaendelea kuhusu miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Mhe. Yong amesema nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuwa nchi hizo zina mahitaji yanayofanana.
Aidha, Mhe. Yong amesema kuwa Singapore inatumia zaidi gesi asilia kama chanzo cha nishati ingawa pia inatumia umeme unaozalishwa kwa maji, jua na upepo ,hivyo Singapole ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati.
Na Mwandishi wetu .
0 Comments