Tarura yatatua changamoto daraja Gairo


WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Gairo Mkoa wa Morogoro, imetekeleza agizo la Rais Dk Samia Suluhu Hassan la kujenga daraja la mawe la Lebenya lenye urefu wa mita 45.

Daraja hilo linalounganisha Wilaya za Kilindi, Gairo na Kilosa linajengwa kwa kutumia fedha zilizobaki wakati wa ujenzi wa daraja la Berega.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum), Kapt. George Mkuchika amesema hayo alipokagua hatua za ujenzi wa daraja hilo ambao umefikia 75% kukamilika.

Mkuchika amesema Rais Samia ametoa mabilioni ya fedha ili kurejesha mawasiliano kwa wananchi kwa kujenga upya madaraja yaliyoharibiwa na mvua zilizonyesha mwaka jana ambazo ziliathiri miundombinu ya barabara katika maeneo mengi nchini.

“Nimefurahi agizo la Rais Samia limetekelezwa, hapa mnajengewa daraja tena mawe tupu, daraja hili litakapokamilika litasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa hapa”, amesema.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Gairo, Mhandisi Simon Masala amesema sh bilioni 1.3 zilizobaki kwenye ujenzi wa daraja la Berega zitumike kuboresha barabara ya Berega – Kinyolisi – Makuyu Km 18, ujenzi wa daraja la mawe na maboksi kalavati ambapo ujenzi wa daraja unatarajiwa kukakamilika Mei 15, 2025.

Amesema daraja hilo linagharimu sh milioni 373 ambapo kukamilika kwake litanufaisha kata saba zenye jumla ya wakazi 766,507 na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya wakazi wa wilaya za Gairo, Kilosa na Kilindi.


Mwandishi : Abel  Mahenge 

Mhariri : Ellukagha Kyusa 



Post a Comment

0 Comments