Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi imetangaza kuanza kukusanya maoni ya wadau, wakiwamo Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora).
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue amesema hayo Octoba 22,2024 Ikulu, Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari ambapo amesema tume imeanza kazi, na sasa iko tayari kuwasikilza wadau ikiwemo, vyama vya kitaaluma, jumuiya za biashara na makundi mengine.
"Tunapenda kuwajulisha wananchi kuwa tume imeanza kazi na sasa iko tayari kushirikiana na kumsikiliza kila mdau, iwe mmoja mmoja au kupitia vyama vya kitaaluma, jumuiya za biashara na makundi mengine" alisema
Aidha Balozi Sefue amesema Tume imeandaa namna bora ya kuratibu ushiriki wa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo, diaspora na wadau wote ili kutoa maoni na mapendekezo.
"Mifumo iliyoandaliwa kwa ajili ya kupokea maoni hayo ni pamoja na kiunganishi cha edodoso.gov.go.tz kwa kutumia namba ya dodoso 54497, barua pepe tume@taxretorm.go.tz na maboresho.kodi@taxreform.go.tz au kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi za 0748 755 677 na 0738 588 813"
Balozi Sefue amesema watafanya mikutano na wananchi katika maeneo mbalimbali na kukutana na wawakilishi wa makundi na kutoa wito kwa taasisi za elimu ya juu, wautafiti na makundi mengine yanaoweza kuandaa mijadala wawasiliane na tume.
Pia ametoa wito kwa vyombo vya habari kuandaa majukwaa ya majadiliano kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi kisha kuandaa taarifa ambazo zitasaidia tume katika utekelezaji wa jukumu hilo na kuwaomba wananchi kutumia fursa hiyo adhimu kutoa maoni kuhusu changamoto na mapendekezo ya maboresho ya mifumo ya kodi na ukusanyaji wa mapato .
“Kodi ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani. Rais Samia ameonesha utashi wa kisiasa wa kushughulikia changamoto hizo na hatua ya kwanza ni kufanya tathmini ya kina ya mfumo ulioko ili kuwa na msingi wa kufanya maboresho ambayo ni wazi yanahitajika,” alisema.
Balozi Sefue alisema katika kipindi cha miama mitatu iliyopita, pato halisi la taifa limekua kwa wastani wa asilimia 4.7, huku mapato ya kodi yakifikia wastani wa asilimia 12.1 ya pato la taifa.
Tume hiyo imeundwa kutokana na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu kero zinazotokana na mfumo wa kodi nchini.
Mwandishi:Harieth Kamugisha
0 Comments