Wizara afya ya Lebanon imethibitisha kuuawa kwa watu 22 na wengine 117 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Israel katikati mwa mji wa Beirut nchini humo.
Shambulizi hilo limefanyika usiku wa kuamkia Oktoba 11,2024 katika mji wa Beirut huku Magari ya kubeba wagonjwa yakiwakimbiza majeruhi kadhaa katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Marekani.
Vyombo vya habari mbalimbali nchini Lebanon vimeripoti kuuawa kwa Msemaji kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah katika shambulizi hilo huku ofisi ya vyombo vya habari vya Hezbollah ikiwa haijatoa taarifa yoyote juu ya shambulizi hilo.
Mashambulizi hayo ya Israel yalilenga majengo ya makazi katika vitongoji viwili vya Bachoura vyenye watu wengi, Nweiri na Basta.
Hii ni mara ya tatu kwa Israel kufanya mashambulizi ya anga katika mji huo ulioko nje ya kitongoji cha kusini cha Dahieh, na kuwaua makamanda wa Hezbollah na kuharibu maeneo yenye silaha.
Wakati huohuo Shirika la habari DW limesema Israel inakabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya vikosi vyake leo ,kukishambulia kituo cha uchunguzi cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) kilichopo katika mji wa Naqoura kusini mwa Lebanon na kuwajeruhi watu wawili. pia inatajwa kuwa vikosi vya Israel viliingia kinyume cha sheria kwenye eneo jingine linalosimamiwa na UNIFIL na ambalo lilishambuliwa siku ya jana Octoba 10,2024 Alhamisi.
Mwandishi: Ramadhan Zaidy
Mhariri: Harieth Kamugisha
0 Comments